Na Mwandishi Wetu, Moshi
VIONGOZI wa dini kutoka ukanda wa kaskazini unaojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga wameibua hoja saba muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kutumia busara katika kipindi hiki nyeti kwa Taifa.
Viongozi hao walikutana katika Kongamano la Amani lililofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) – Uhuru Hosteli, Moshi. Washiriki walikuwa ni maaskofu, masheikh, mapadri, wachungaji pamoja na viongozi wa kamati za dini za vijana na wanawake.
Akisoma maazimio ya kongamano hilo, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kilimanjaro, Alhaj Awadh Lema, alisema viongozi hao wamekubaliana kuhamasisha wapiga kura kuhakiki taarifa zao na kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Pia wameazimia kuendelea na makongamano ya amani kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha, viongozi hao wameitaka vyombo vya dola kutumia hekima na busara katika utekelezaji wa majukumu yao hasa siku ya uchaguzi, huku wakisisitiza viongozi wa dini kuwaelimisha waumini kuhusu haki na wajibu wao katika kulinda amani. Wamekemea vikali vitendo vya uchochezi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, wakipendekeza pia ushiriki mpana wa viongozi wa dini katika vyombo vya maamuzi na utungaji wa sheria. Wamehimiza kila mwananchi kutambua kuwa kulinda amani ni wajibu wake, hata anapodai haki.
Sheikh Shaban Mlewa, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisema amani ni tunu adimu ambayo ikipotea ni vigumu kuirudisha, akitoa mfano wa nchi zilizojikuta kwenye machafuko baada ya uchaguzi.
“Ni muhimu Watanzania kuwa wazalendo, kupendana, kusameheana na kuwa waadilifu ili kuendeleza utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Sheikh Shaban Juma, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, alieleza kuwa hakuna haki bila amani, akisisitiza kuwa msingi wa amani ni kumtambua Mungu, kutambua thamani ya nafsi yako na kulinda haki za wengine.
Wakili Mchungaji Daniel Swai, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini, alihimiza kila Mtanzania kutimiza haki yake ya kupiga kura na kulinda haki hiyo kwa njia ya amani.
“Ni kosa kubwa kuhamasisha watu kutotimiza wajibu wao wa kikatiba. Haki na amani ni mambo yanayokwenda pamoja,” alieleza.
Padri Deogratias Matiika, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Moshi, alisema haki ni msingi wa maendeleo ya taifa. Alisisitiza heshima kati ya wananchi na viongozi, na kukemea tabia ya kutoa matusi kwa viongozi kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Padri Francis Mahimbo kutoka Kanisa la Anglikana – Dayosisi ya Tanga, alihimiza kujengwa kwa jamii yenye kuvumiliana, akisema:
“Msingi wa amani ni haki. Taifa lisilolinda haki za watu wake haliwezi kuwa na utulivu wa kweli.”
Katika kongamano hilo, viongozi wa kamati za dini za wanawake na vijana walitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki uchaguzi kwa utulivu, kujiepusha na vurugu na kuwakataa wale wanaochochea uvunjifu wa sheria, wakisisitiza kuwa amani ni urithi wa pamoja unaopaswa kulindwa na kila mmoja.