NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Baada ya kufanya mkutano mkubwa wa kampeni katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana, ambapo alisisitiza kuwa yeye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu aliyeapa kuilinda Katiba ya nchi, leo Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea na kampeni zake katika eneo la Kinyerezi, Wilaya ya Ilala.
Katika mkutano wa jana, Dkt. Samia aliwahimiza Watanzania kujitoa kwa wingi kwenda kupiga kura kwa amani tarehe 29 Oktoba, akisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kidemokrasia na unapaswa kufanyika kwa utulivu bila hofu wala vurugu.
“Mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania, nimeapa kuilinda Katiba na kuhakikisha nchi inabaki salama. Nawaomba Watanzania mjitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani, kisha mrudi majumbani mkasubiri matokeo kwa utulivu,” alisema Dkt. Samia.
Leo, katika mkutano wa Kinyerezi, maelfu ya wananchi wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo kubwa, lililoandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam, kama sehemu ya mwendelezo wa kampeni zake jijini humo.
Dkt. Samia anatarajiwa kuzungumzia mipango ya maendeleo ya Dar es Salaam ikiwemo kuboresha barabara na usafiri wa umma, upatikanaji wa maji safi, makazi bora, ajira kwa vijana, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na usimamizi wa taka mijini, mambo ambayo yamepewa uzito katika Ilani ya CCM 2025–2030.



