NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba, amesema kuwa zaidi ya asilimia 65 ya jimbo hilo linapitiwa na mito, na baadhi ya mito kama Mto Ngombe ilikuwa ikitesa wananchi wa Magomeni, Tandale, Ndugumbi na Hananasifu kutokana na ukosefu wa fidia na malipo kwa wakandarasi wakati serikali ilipoanza kazi.
Ameyasema hayo Oktoba 21, 2025 jijini Dar es Salaam katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia, wananchi wameshalipwa fidia, na kazi za kuondoa tatizo la mafuriko zinaendelea. Pia amebainisha kuwa ujenzi wa daraja la Jangwani na Mzimuni pamoja na flyover tatu unalenga kuboresha miundombinu, kufungua fursa za kibiashara na kuongeza maendeleo kwa watoto.
Aidha amebainisha kuwa miradi ya barabara imepanuliwa, vituo vya afya vya kisasa vimeimarishwa, na masoko ya Kinondoni yameweza kuhudumia wananchi elfu tatu kwa siku, jambo linaloongeza fursa za biashara na kipato cha wananchi.
Aidha amebainisha kuwa nyumba ambazo hazijapimwa na zilizokuwa kwenye maeneo hatarishi zimeondolewa, na wananchi wanatakiwa kupatiwa hati ili kujiendeleza vizuri na kupunguza umaskini.
Pia, amebainisha kuwa bwawa la Kidunda litaleta ukombozi kwa uhaba wa maji hasa wakati wa jua kali, na kuomba serikali iendelee kuwekeza fedha.
Tarimba amewaomba wananchi kumpigia kura Dkt. Samia, yeye kama Mbunge, pamoja na madiwani wote wa Jimbo la Kinondoni.