Na Meleka Kulwa- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura Yunus, amesema kuwa Serikali itaanzisha Mfuko wa Dhamana kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo, na Benki ya Ushirika ili kuwawezesha wakulima na wananchi wengine wanaojishughulisha na uongezaji wa thamani kwa mazao ya kilimo, mifugo na samaki kukopa katika taasisi za fedha kwa riba ndogo.
Amesema hayo Oktoba 21,2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa Wakulima na Wazalishaji Wadogo katika Sekta ya Kilimo kwa mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Mbeya yanayofanyika katika ukumbi wa Jenerali Venance Mabeyo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoa mafunzo kwa wakulima na wazalishaji wadogo ili kuongeza tija katika uzalishaji na ubora wa bidhaa.
Aidha, amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imedhamiria kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima 1,000 kwa kushirikiana na TARI, ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kukuza pato la taifa.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita zaidi katika vitendo na yatahusu mazao ya zabibu kwa Mkoa wa Dodoma, alizeti kwa Singida, nyanya na mchicha lishe kwa Iringa, pamoja na maharage, parachichi na matumizi ya mashine za kilimo kwa Mkoa wa Mbeya.
Pia, Amesema kuwa katika kipindi cha Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo cha kibiashara na kuimarisha upatikanaji wa teknolojia.
Aidha, amebainisha kuwa sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa taifa, ikichangia asilimia 26.5 ya Pato la Taifa, kuajiri takribani asilimia 65 ya nguvukazi nchini na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.
Amebainiaha kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima na wazalishaji wadogo wanawezeshwa kupata ujuzi, mitaji na masoko ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wananchi.
Aidha, amewapongeza washiriki wa mafunzo kwa kupata nafasi hiyo na kuwataka kutumia ipasavyo fursa waliyopewa kujifunza kwa bidii ili wawe mabalozi wa mabadiliko katika maeneo yao.
Pia, Ameishukuru TARI, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na wadau wengine kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuratibu na kufanikisha mafunzo hayo.