Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa majimbo ya Kinondoni, Kibamba, Kawe na Ubungo katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi za CCM zilizofanyika kwenye viwanja vya Leaders Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Oktoba, 2025.
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi Ilani ya Uchaguzi baadhi ya wagombea Ubunge wa Majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Leaders Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Oktoba, 2025.
NA JOHN BUKUKU – DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewatoa hofu Watanzania akisisitiza kuwa hakuna tishio lolote la kiusalama wakati wa uchaguzi mkuu, na kwamba maandamano pekee yatakayokuwepo ni yale ya wananchi kuelekea vituoni kupiga kura kwa amani.
“Niwahakikishie tarehe 29 mwezi huu wa 10, niwaombe tokeni mwende mkapige kura. Ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda kupiga kura, na hakuna tishio lolote la kiusalama nchini. “Anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi. Niwaombe ndugu zangu twendeni mkapige kura. Baba ukitoka hakikisha umetoka na familia yako, mabalozi hakikisheni mnawatoa watu wenu wote mkapige kura. Tukaiheshimishe Tanzania, tukaiheshimishe Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Dkt. Samia alisisitiza kuwa anaendelea kutekeleza kiapo chake cha kulinda nchi, kujenga utu na kuheshimisha utu wa Mtanzania. “Niliapa kuilinda nchi, kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha utu wa Mtanzania, na ndicho ninachokifanya,” alisema.
Alibainisha kuwa hatua mbalimbali za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi, elimu, afya, umeme na usalama ni sehemu ya kuimarisha utu wa Mtanzania. “Sina uchungu wa kubeba matusi yanayotolewa kwa sababu nafanya kazi hii. Sina uchungu hata kidogo wala sijutii. Niachieni mengine, matusi nayabeba kwa niaba yenu,” alisema Rais Samia.
Akitoa mifano ya viongozi wa kiroho waliopitia changamoto kwa ajili ya watu, alisema: “Manabii wetu Bwana Yesu alisulubiwa kwa amri ya Mungu ili kukomboa watu. Nabii Muhammad alipigwa hadi kutolewa meno kwa ajili ya kukomboa watu. Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania na ndicho ninachokifanya.”
Rais Samia alisisitiza kuwa hakuna sababu ya hofu wakati wa uchaguzi, akibainisha kuwa: “Kama nilivyosisitiza, hata kibati cha soda hakitapasuka. Twendeni tukapige kura.”
Katika hotuba hiyo, Dkt. Samia pia aligusia maendeleo makubwa ya miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam, ikiwemo mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT).
Alisema kuwa katika kipindi chake cha uongozi, serikali imejenga kilometa 94.9 za miundombinu hiyo kwa gharama ya Sh trilioni 2.1. “Serikali inakwenda kukamilisha barabara zote za mradi wa BRT huku ikishirikisha sekta binafsi,” alibainisha.
“Tayari tumepata watoa huduma – kampuni ya ENG yenye mabasi 177, awamu ya pili kampuni ya Mofat yenye mabasi 255, YG Link yenye mabasi 166, na Metro Link City yenye mabasi 334,” alifafanua.
Aliongeza kuwa kuanzia Januari mwakani, wakazi wa Dar es Salaam watashuhudia mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za usafiri kupitia mradi huo wa BRT.
Rais Samia alibainisha kuwa mradi huo umeipa Tanzania sifa kubwa kimataifa kutokana na usimamizi na ubunifu wake. “Niwahakikishie wakazi wa Kinondoni, Ubungo na Dar es Salaam kwa ujumla, mageuzi haya tutayalinda. Mradi huu utaleta mapinduzi ya usafiri ndani ya jiji,” alisema.
Aidha, aliwahakikishia wamiliki wa daladala kuwa serikali imekamilisha ujenzi wa stendi ya Mwenge na itaendelea kuboresha stendi za Kawe, Bunju B na Tegeta Nyuki ili kutoa nafasi bora za utoaji huduma.
Akihitimisha, Rais Samia alisema serikali inaendelea kutekeleza matamko ya kimataifa kuhusu maendeleo jumuishi ikiwemo tamko la Milenia na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Tumetengeneza mipango mahsusi kwa watu wenye ulemavu katika elimu, afya na upatikanaji wa huduma serikalini. Hatuachi mtu nyuma — tunatekeleza matamko haya kwa vitendo,” alisisitiza Dkt. Samia