Na Silivia Amandius
Bukoba,Kagera.
Wakazi wa Mkoa wa Kagera wamepata neema ya huduma za kibingwa baada ya madaktari bingwa na wauguzi wabobezi 48 kutoka programu ya Mama Samia Mentorship kuanza kambi ya siku tano ya matibabu katika halmashauri zote nane za mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba, Kiongozi wa timu hiyo kutoka Wizara ya Afya, Dk. Patrick Kushoka, alisema madaktari hao wanahusisha kada mbalimbali zikiwemo magonjwa ya wanawake na uzazi, usingizi na ganzi, upasuaji, magonjwa ya watoto, meno, mkojo, pamoja na magonjwa ya ndani kama shinikizo la damu na kisukari.
Dk. Kushoka alibainisha kuwa pamoja na kutoa huduma kwa wananchi, wataalamu hao pia watajenga uwezo kwa wataalamu wa afya wa ndani wa halmashauri hizo ili kuboresha utoaji huduma kwa muda mrefu.
“Tutaendelea kutoa huduma katika halmashauri zote nane za Kagera. Wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kwani hata huduma za upasuaji zitafanyika katika vituo vyetu husika,” alisema Dk. Kushoka.
Kabla ya kuelekea vituoni, madaktari hao walipata fursa ya kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ambapo walisisitiza dhamira yao ya kuhakikisha wananchi wote wanapata matibabu bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk. Samuel Laizer, alisema kuwa hii ni mara ya nne madaktari hao kutoa huduma hizo mkoani humo, na katika awamu tatu zilizopita zaidi ya wananchi elfu sita walihudumiwa.
“Huduma hizi zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu, hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni. Zinapunguza gharama na muda wa kusafiri kutafuta huduma za kibingwa nje ya mkoa,” alisema Dk. Laizer.
Huduma hizo zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa wiki hii, zikiwa na lengo la kugusa wananchi wengi zaidi katika maeneo yote ya Mkoa wa Kagera.