NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anachukizwa na wananchi kubambikiziwa bili za maji huku akiwaeleza wasoma mita nchini kwamba jambo hilo limepitwa na wakati, na maelekezo ya Serikali ni kwenda kutumia mfumo wa Luku kama ilivyo kwa umeme.
Aweso aliyasema hayo leo wakati akizungumza katika mkutano wa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu, uliofanyika katika eneo la Leaders, Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ambapo alisema maelekezo ya Wizara ya Maji ni kwamba ni haki ya wananchi kupata maji, na Dkt. Samia amesisitiza kuchukizwa na ubambikizwaji wa bili za maji.
“Nataka kuwaambia wasoma mita, hizo ni za zamani. Dkt. Samia ametuagiza twende kwenye mfumo wa Luku kwenye maji kama umeme. Huu utakuwa mwarobaini mkubwa. Niwaambie, Dkt. Samia ametuvusha kwenye nyakati zote, na aina yake hapatikani kila wakati. Tumempata, tumtumie. Niwaombe wana Dar twendeni Oktoba tukatiki kwake, wabunge na madiwani wa CCM,” alisema.
Aidha, alisema wameendelea kuboresha huduma kwa wateja ambapo wananchi wanaotakiwa kuunganishiwa maji hawapaswi kusubiri zaidi ya siku saba, jambo lililosaidia kuondoa changamoto zilizokuwepo awali.
Aweso alisema Dkt. Samia ameweka jicho lake Dar es Salaam akitambua kuwa maji ni huduma muhimu. “Maji ni siasa, Dar ikipiga chafya nchi inapata mafua,” alisema, akiongeza kuwa hivi karibuni alitumiwa ujumbe binafsi kuhusu changamoto ya maji kwa mtu mmoja na baada ya kufuatilia, huduma ilirejeshwa mara moja.
Alisema Jiji la Dar es Salaam lina mahitaji ya maji lita milioni 684, huku mitambo ikizalisha lita milioni 534. “Hizo ni jitihada zako Dkt. Samia. Najiuliza ingekuwaje kama si uwekezaji wako kwenye maji hapa Dar? Uzuri wa maji ukikosekana utaambiwa hayapo. Dkt. Samia apewe heshima yake kwa kazi kubwa aliyoifanya,” alisema.
Aweso aliongeza kuwa maeneo ya Kusini mwa Dar es Salaam, kama Ukonga na Segera, yamenufaika na ujenzi wa tenki kubwa la maji. “Nataka kuwaambia, Dar Dkt. Samia ndiye suluhisho la matatizo ya maji ya Dar na Watanzania,” alisema.
Alibainisha kuwa Rais Samia ni kiongozi wa vitendo na sio maneno, na kwamba ametoa shilingi bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa pampu kubwa nane zitakazofungwa ili kuhakikisha hakuna mtu anayekosa maji.
Aweso alisema Dkt. Samia amelipa kipaumbele Jiji la Dar es Salaam kwa miaka 25 ijayo, akilitambua kama kitovu cha biashara na uchumi wa nchi. Amesema serikali inajenga bwawa la Kidunda, ndoto ya muda mrefu ya Baba wa Taifa.
Alisema maamuzi hayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara bungeni, na kwamba Rais amesema “inatosha” — serikali itajenga bwawa hilo kwa fedha zake wenyewe. Zaidi ya Shilingi Milioni 336 zimetolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu, na mkandarasi yupo eneo la kazi ambapo utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 32.
“Mhe. Mgombea, sisi tunakuombea mema. Oktoba unakwenda kupata ushindi wa kimbunga. Maamuzi haya utakumbukwa milele na milele. Sisi tutaendelea kuboresha huduma kwa wateja,” alisema Aweso.
Waziri Aweso alisema eneo linalowasumbua zaidi Wizara ya Maji ni Kibamba na Ubungo, na kwamba Rais Dkt. Samia hataki kusikia tena habari za changamoto za maji. “Mitambo inazalisha kwa wingi, maji yafike kila sehemu. Rais ametoa Sh. Bilioni 3.2 kujenga tenki lenye ujazo wa lita milioni 6. Leo Kibamba na maeneo mengine wanapata maji safi na salama,” alisema.
Aliongeza kuwa Jimbo la Kibamba lina mitaa 52 na hakuna mtaa ambao haujafikiwa na mtandao wa maji. Wizara imeweka mfumo bora wa mawasiliano kati ya jamii, viongozi na wananchi, jambo lililosaidia kutatua changamoto ndogo kama presha ndogo za maji.
Aweso alisema wamekuwa wakikutana na wabunge na wenyeviti wa mitaa kutoa taarifa za changamoto hizo, na pale inapojitokeza tatizo la presha au bomba, mafundi wanashughulikia mara moja ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.