Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 21, 2025 jijini Dar es Salaam.
……………
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watu 89 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambapo dawa zenye jumla ya kilogramu 10,763.94, pamoja na lita 153 za kemikali bashirifu, zimekamatwa katika operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 21, 2025, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema miongoni mwa mafanikio ya operesheni hizo ni pamoja na kugundua mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya kimataifa.
Katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, kilo 40.32 za mirungi zilizokaushwa na kufungwa kwenye paketi 80 zenye maandishi ya Dry Basil Leaves zilinaswa zikisafirishwa kwenda Canada na Italia kupitia kampuni za usafirishaji.
Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Yusuphu S. Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41), ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa mirungi hiyo iliingia nchini kwa njia zisizo halali kutoka nchi jirani.
“Uchunguzi umeonesha kuwepo kwa mtandao unaojumuisha baadhi ya waendesha bodaboda na mawakala wa usafirishaji, jambo linalohatarisha usalama wa taifa na kuhujumu taswira ya nchi kimataifa,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo, akiweka wazi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waliohusika.
Katika operesheni nyingine iliyofanyika Mlalakuwa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kundi la vijana wanne limekamatwa kwa kutengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya sherehe ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Watuhumiwa hao ni Bright A. Malisa, Humphrey G. Safari, Novatus A. Kileo na Chriss P. Mandoza, wote wenye umri wa miaka 26.
Katika tukio hilo, biskuti 140 za bangi, puli nane, na pakiti tisa za bangi zenye uzito wa kilo 2.858 zilipatikana.
“Matumizi ya dawa za kulevya kwa visingizio vya burudani ni tishio kwa afya ya vijana na maendeleo ya taifa. Tunatoa wito kwa vijana kuepuka makundi yenye mienendo potofu na kujikita katika shughuli halali za kujenga maisha yao,” amesema Lyimo.
Aidha, Kamishna Jenerali huyo amesema uchunguzi maalum unaendelea kuhusu matumizi ya bangi katika bidhaa kama vyakula, vinywaji, vipodozi na sigara za kielektroniki (vapes), ambavyo baadhi vimebainika kuwa na viambata vya dawa hizo.
Katika operesheni nyingine zilizotekelezwa kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye mikoa mbalimbali, zilikamatwa kilo 9,164.92 za bangi, kilo 1,555.46 za mirungi, gramu 367 za skanka, na gramu 7.498 za heroin. Pia, ekari 11.5 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.
Kamishna Jenerali Lyimo amesisitiza kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya si tu vinaharibu afya bali vinaathiri uchumi na kuhatarisha usalama wa taifa.
Ameeleza kuwa mafanikio haya yanatokana na mshikamano imara kati ya DCEA na vyombo vingine vya dola katika kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kupambana na biashara hiyo haramu.
Aidha, amewataka waendesha bodaboda, mawakala na wamiliki wa kampuni za usafirishaji kuwa makini na mizigo wanayosafirisha.