NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Mgombea ubunge kupitia NGOs, Asha Baraka, amesema kuwa ujio wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika mkutano wa kampeni unaofanyika kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ni ishara ya umoja na amani nchini.
Ameyasema hayo Oktoba 21, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa Watanzania wote wanapaswa kutokuwa na woga na watumie haki yao ya kikatiba kushiriki katika uchaguzi kwa kumchagua Rais, Mbunge na Diwani. Amebainisha kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kimbilio la watu kutoka mataifa jirani kama Burundi, Congo, Zambia, Malawi na Rwanda, hivyo ni wajibu wa Watanzania kudumisha amani na uzalendo.
Aidha, amebainisha kuwa maandamano si sehemu ya utamaduni wa Watanzania, kwani mara nyingi watu hukusanyika kwa furaha kupitia michezo na burudani. Amehimiza umuhimu wa kulinda mali za nchi, kushiriki kwenye michezo, na kuendelea kuunga mkono juhudi za Dkt. Samia ambaye ametoa motisha kubwa katika mashindano ya kimataifa.
Amesema kuwa ni muhimu Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura kumchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka vijana kuacha kushawishika na taarifa za upotoshaji zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Mwamini Hassan, mkazi wa Ubungo, amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi wa kwanza wa kike aliyefanya mambo makubwa kwa taifa, na amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kumchagua.
Aidha, amebainisha kuwa vijana wanapaswa kuacha kusikiliza maneno ya mitandaoni yanayohamasisha uvunjifu wa amani, badala yake waende kupiga kura na kuendelea kuona matokeo ya kazi nzuri za Dkt. Samia.