Na Meleka Kulwa -Dodoma
Tume ya Utumishi wa Umma imepokea jumla ya rufaa na malalamiko 108 kutoka kwa watumishi wa umma nchini, ambapo makosa yanayoongoza ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma, utoro kazini, kughushi vyeti, kutoa taarifa za uongo, uzembe kazini na wizi wa mali za umma.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Tume hiyo, Bw. John Mbisso, alipokuwa anazungumza na waandishi wa Habari Oktoba 20,2025 jijini Dodoma,
Katika taarifa iliyotolewa kufuatia mkutano wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/26 wa tume hiyo uliofanyika chini ya Mwenyekiti Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, imeelezwa kuwa tume hiyo ilijadili na kufanya maamuzi juu ya rufaa na malalamiko hayo yaliyowasilishwa na watumishi kutoka kada mbalimbali.
Maamuzi ya Rufaa na Malalamiko,Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso, alifafanua kuwa kati ya rufaa 93 zilizowasilishwa,Rufaa 34 zimekubaliwa bila masharti,Rufaa 9 zimekubaliwa kwa masharti ya kuanza upya kwa mamlaka za nidhamu husika,Rufaa 38 zimekataliwa ,Rufaa 10 zilitupiliwa mbali kwa sababu ziliwasilishwa nje ya muda wa kisheria,Kuhusu malalamiko 15 yaliyowasilishwa,
Aidha, alibainisha kuwa kada zilizowasilisha rufaa na malalamiko kwa wingi ni kutoka mamlaka za serikali za mitaa.
Bw. Mbisso amesema kuwa Malalamiko 6 yalikubaliwa,Malalamiko 6 yakakataliwa,Malalamiko 3 yalitupiliwa mbali
Pia, watumishi walilalamikia kuchelewa kupandishwa vyeo au kutopandishwa kabisa, pamoja na kuondolewa kazini kinyume cha sheria.
Upande wa Malalamiko ya Watumishi, yaliyotajwa ni pamoja na kutolipwa stahili zao na waajiri wao, ikiwemo mishahara, posho za uhamisho, na stahili nyingine za kisheria.
Kwa upande wake Afisa wa Sheria wa Tume hiyo, Bw. Hussein Mussa, alieleza kuwa tume ina mamlaka ya kurudisha mashauri kwa mamlaka husika kusikilizwa upya endapo haki ya msingi haikuzingatiwa, kwa mujibu wa kifungu cha 62(4) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Bw. Mbisso amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili, sheria na taratibu za utumishi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha Mbisso amesema Katika mkutano huo, warufani 18 na warufaniwa 3 walipewa nafasi ya kufika mbele ya tume kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zao za rufaa na majibu ya hoja hizo.
Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ufuatiliaji wa haki za watumishi wa umma kwa mujibu wa sheria, ili kuhakikisha utumishi wa umma unazingatia misingi ya uwazi, haki na uwajibikaji.