Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeshiriki kongamano la wafanyabiashara wadogowadogo lililofanyika leo Oktoba 20, katika ukumbi wa KCU, Bukoba, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kutumia huduma za dawati maalumu la elimu ya kodi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Uwezeshaji Biashara wa TRA Mkoa wa Kagera, Bi Agnes Kimbondile, kutoka dawati la wafanyabiashara wadogowadogo, amewataka wafanyabiashara hao kutumia ipasavyo dawati hilo ili kuboresha biashara zao na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kodi.
Bi Kimbondile amesema kuwa dawati hilo limeanzishwa mahsusi kusaidia wafanyabiashara wadogowadogo kupata ushauri wa kitaalamu, taarifa sahihi kuhusu kodi, na namna bora ya kuendesha biashara kwa kufuata taratibu za kisheria.
Aidha, ameongeza kuwa kupitia dawati hilo, wafanyabiashara watakuwa karibu zaidi na TRA na hivyo kurahisishiwa huduma mbalimbali, hatua ambayo itachangia kukuza biashara na kuongeza mapato ya serikali kwa maendeleo ya taifa.