NA JOHN BUKUKU- KIBITI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo mabwawa, skimu za umwagiliaji, viwanda na uvuvi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Ujamaa, Ikwiriri, wilayani Kibiti mkoani Pwani, Oktoba 20, 2025.
Dkt. Samia amesema kuwa serikali imepanga kujenga mabwawa makubwa mawili ya Mbakimtuli na Ngorongo, sambamba na skimu ya umwagiliaji ya hekta 13,000 katika bonde la Kisarawe, kati ya hekta 60,000 zinazotarajiwa kumwagiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, amesema kuwa serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa tuta la kuzuia mafuriko, ambapo mkandarasi tayari amepatikana kwa gharama ya shilingi bilioni 245, pamoja na ujenzi wa kilomita 90 za barabara na makalavati ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya wakulima.
Katika sekta ya viwanda, Dkt. Samia amesema kuwa wawekezaji wameanza kuonesha nia ya kuwekeza Rufiji, hatua itakayoongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wa uvuvi, amesema kuwa serikali imeleta boti mbili kubwa za doria ambazo zimepunguza uvuvi haramu kutoka asilimia 70 hadi 30, na kuongeza uzalishaji wa samaki kutoka tani 610,000 hadi tani 900,000.
Aidha, amebainisha kuwa ujenzi wa kiwanda cha kusindika samaki katika Kata ya Ikwiriri unaendelea, huku CCM ikiahidi kujenga mabwawa mengine matano ya ufugaji wa samaki katika kata za Utete, Mbwara, Ikwiriri, Mkongo na Ngorongo.
Pia, amesema kuwa serikali imeanzisha ranchi ndogo za mifugo katika kata za Tumbi na Mtwara, pamoja na kuongeza minada ya mifugo katika maeneo ya Nyamwage na Umwe Kusini, ambayo ujenzi wake unaendelea.
Aidha, Dkt. Samia amebainisha kuwa mfumo wa asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeboreshwa ili fedha ziwafikie walengwa, ambapo Rufiji imenufaika na shilingi bilioni 3.42 zilizotolewa kwa vikundi 502.
Pia, amesema kuwa miradi hiyo yote inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi, huku akisisitiza kuwa kazi ya CCM ni kufanya kazi na kujenga utu wa mtu.