NA JOHN BUKUKU- PWANI
Baada ya kufanya mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa ya nyanda za juu magharibi, leo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuendelea na mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa ya Pwani, hususan katika Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri.
Maandalizi ya mapokezi katika maeneo hayo yamepamba moto, huku maelfu ya wananchi wakijitokeza mapema asubuhi kuandaa maandamano ya kumpokea kiongozi huyo ambaye anazunguka nchi nzima kuomba ridhaa ya kuongoza kwa muhula mwingine kupitia ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.
Wananchi wa maeneo hayo wameonesha shauku kubwa, wakisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia imeleta mabadiliko makubwa katika sekta za kilimo, elimu, afya, maji na miundombinu, ambazo zimechochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Pwani.
Katika mikutano hiyo ya leo, Dkt. Samia anatarajiwa kuzungumza na wananchi kuhusu dira ya maendeleo endelevu, akisisitiza umuhimu wa umoja, amani na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Aidha, amekuwa akihimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, na baada ya kupiga kura kurudi majumbani kwa amani wakisubiri matokeo, kama ishara ya ustaarabu na upendo kwa taifa.
Kauli mbiu inayosikika katika maeneo mbalimbali ni “Tunaendelea na Mama hadi 2030”, ikibeba ujumbe wa matumaini, umoja na maendeleo kwa Watanzania wote.