Oktoba 20, 2025
Asha Madamde, maarufu kama Bibi Hatibu mwenye miaka 120 ,mkazi wa mtaa wa Msufini, kata ya Sofu, Kibaha Mjini mkoani Pwani, amesisitiza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 huku akimuombea dua mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt .Samia Suluhu Hassan.
Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 120, Bibi Hatibu amesema kuwa afya yake na nguvu za Mungu zimemuwezesha kuendelea kushiriki katika shughuli muhimu za kijamii, ikiwemo kutimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura.
Bibi huyo amemuombea dua Dkt Samia na kuitakia mafanikio makubwa CCM wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba inayoongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Kibaha Mjini, Elina Mgonja, pamoja na kamati ya utekelezaji ya UWT.
Bibi Hatibu ameeleza, amani ni tunu ya Tanzania, na uchaguzi ni suala nyeti kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Nae Elina Mgonja, Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, amemshukuru Bibi Hatibu kwa dua yake kwa mgombea urais Dkt. Samia na kusema kwamba anastahili ushindi wa kishindo kutokana na kazi kubwa aliyofanikisha katika kipindi chake cha uongozi.
Kampeni hizo zinaendelea lengo kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana na kueleza mipango ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030.