Na Silivia Amandius
Ngara:
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ngara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dotto Jasson Bahemu, amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa amani na utulivu. Amesema ni muhimu kila mwenye sifa ya kupiga kura kutumia haki yake ya kikatiba kuchagua viongozi wanaofaa kuongoza nchi katika ngazi za urais, ubunge na udiwani.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Bukiriro, Bahemu amewaomba wananchi waendelee kuiamini CCM kwa kuwachagua wagombea wake wote, akiwemo Mgombea Udiwani wa Kata ya Bukiriro, Erick Emily Nkilamachumu, Mgombea Ubunge Dotto Jasson Bahemu, na Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bahemu amesema kuwa zoezi la kupiga kura ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania, hivyo wananchi hawapaswi kukosa kushiriki katika uchaguzi huo muhimu. Amesisitiza kuwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kutasaidia kuhakikisha maendeleo yanayotekelezwa na serikali ya CCM yanaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.
Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, Bahemu amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi ya maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 81 imetekelezwa katika Jimbo la Ngara pekee, hatua inayothibitisha dhamira ya serikali katika kuinua maisha ya wananchi vijijini na mijini.
Bahemu amewataka wananchi wa Ngara kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi kwa kupiga kura za “ndiyo” kwa wagombea wote wa CCM ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya kijamii, miundombinu na huduma za msingi unaendelea kwa kasi. Ameongeza kuwa ushindi wa CCM ni ushindi wa maendeleo kwa wananchi wote wa Ngara.