Aliyekuwa mtia nia wa Ubunge Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Production, Alex Msama, ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumpokea na kushiriki katika kampeni za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais kupitia chama hicho.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Msama amesema ujio wa Rais Samia katika jiji la Dar es Salaam ni tukio muhimu linaloonesha dhamira yake ya kukutana na wananchi na kuwasikiliza moja kwa moja kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Amefafanua kuwa Rais Samia amekuwa akipokelewa kwa shangwe na hamasa kubwa katika mikoa yote aliyoitembelea, hali inayoonyesha mapenzi makubwa ya wananchi kwake.
“Rais wetu amezunguka katika mikoa mingi na kila alipofika amepokelewa kwa furaha kubwa. Sasa anakuja Dar es Salaam, hivyo ni jukumu letu wakazi wa jiji hili kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumuunga mkono katika kampeni zake ambazo zitafanyika katika maeneo ya Kinondoni, Ilala na Temeke,” amesema Msama.
Aidha, Msama amewaasa wananchi wa dini zote na makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kampeni hizo kwa amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kila mmoja ana wajibu wa kulinda hali hiyo.
“Nchi yetu ni Nchi ya amani kama vyombo vya Ulinzi vilivyo sema uchaguzi utakuwa ni WA amani na utulivu, tuwadharau, tuwapuuze hao ndugu zetu wanaishi katika mataifa ya mbali ambao wanaotaka kutvurugia amani yetu sisi tunaishi Tanzania” amesema Msama