NA JOHN BUKUKU – KATAVI
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa, Ezekiel Wenje, amesema kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani na usalama wa nchi, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Oktoba 18, 2025 mkoani Katavi, Wenje amesema amani ni msingi wa maendeleo na hakuna chama cha siasa kinachopaswa kuchochea vurugu kwa kisingizio cha siasa.
“Nimepata wokovu mpya. Jumapili, asubuhi, mchana na usiku. Lakini tunapokuja kwenye suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu, naamini kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani ya nchi yetu,” amesema Wenje.
Amebainisha kuwa kushiriki uchaguzi ni haki ya kisheria na njia pekee ya kupata madaraka, hivyo vyama vinavyokataa kushiriki uchaguzi vinakosa uhalali wa kulalamika.
“Wamekataa kushiriki uchaguzi ni kiashiria cha kutaka fujo, kwa sababu madaraka yanapatikana kwenye sanduku la kura tu,” amesema Wenje.
Pia, Wenje amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini imefanya vizuri.
“Nashuhudia takwimu za miradi ya maendeleo, ukweli ni kwamba Dkt. Samia anaupiga mwingi kwa maendeleo,” amesema Wenje.
Aidha, amebainisha kuwa Tume ya Uchaguzi ni huru na inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hivyo ni ujinga kuilaumu tume kila mara matokeo yasipowapendeza baadhi ya watu.
“Tume ya Uchaguzi ni huru na ina haki. Watu wakishindwa tume ni mbaya, huu ni ujinga,” amesema Wenje.
Pia, Wenje amewataka Watanzania kuwa hodari na jasiri, akibainisha kuwa hakuna Mungu anayefanya kazi kwa watu wanaokimbia uchaguzi.