NA JOHN BUKUKU
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kufuatia usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa kodi na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Oktoba 18, 2025 mkoani Katavi, Mwigulu amesema kuwa juhudi hizo zimewezesha Serikali kuongeza makusanyo ya mapato kutoka wastani wa takribani trilioni moja kwa mwezi hadi kufikia zaidi ya trilioni tatu.
Amesema kuwa ongezeko hilo la mapato limewezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, zahanati na madarasa nchi nzima. Aidha, amebainisha kuwa tangu uhuru, Tanzania haijawahi kujenga miundombinu ya afya na elimu kwa kiwango kikubwa kama kilivyofanyika katika kipindi cha sasa.
“Tumefanikiwa kujenga wilaya zaidi ya mia moja zenye hospitali, vituo vya afya zaidi ya mia sita, na zahanati zaidi ya elfu mbili na mia nane kote nchini. Hapa Katavi pekee, zahanati mpya zaidi ya hamsini zimejengwa, jambo linaloonyesha matumizi sahihi ya mapato ya Serikali,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, amebainisha kuwa mapato hayo yamechangia pia katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara za vijijini na mikoa, ambapo kwa sasa zaidi ya shilingi bilioni mia nne zimetumika katika Mkoa wa Katavi pekee.
Waziri Mwigulu amesema kuwa kutokana na usimamizi mzuri wa uchumi, Tanzania ina akiba ya fedha za kigeni zaidi ya dola bilioni 6.7, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 16, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya nchi.
Amebainisha kuwa kauli zinazodai Serikali imeishiwa fedha si za kweli na zina lengo la kupotosha umma, akisisitiza kuwa Tanzania ina uchumi imara na usioyumba.
Aidha, Waziri Nchemba ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchochea vurugu au migawanyiko.
“Ukiona mtu anakuelekeza kufanya fujo dhidi ya nchi yako, ujue huyo haitakii mema Tanzania. Tuwe watulivu, tuende tukapige kura kwa amani na utulivu,” amesema Dkt. Mwigulu.
Pia, amesema kuwa uadilifu na uzalendo katika ukusanyaji wa mapato ndiyo siri ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.