Na Mwamvua Mwinyi-Bagamoyo
Oktoba 18, 2025
Mwanamke mmoja aitwaye Mengi Waziri (25), mkulima na mkazi wa Masiwa, Kata ya Dunda, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, amefariki dunia baada ya kugongwa kichwani na mfuniko wa mtungi wa gesi ya kuzimia moto uliolipuka ghafla wakati ukigongwa kwa nyundo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salim Morcase, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa tukio hilo limetokea Oktoba 18, 2025, majira ya saa 5:30 asubuhi katika maeneo ya Masiwa, Kata ya Dunda, Wilaya ya Bagamoyo.
“Mtungi huo wa gesi ya kuzimia moto, unaokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 20, uliokuwa ukigongwa kwa nyundo, ulifyatuka ghafla na mfuniko wake kumpiga kichwani marehemu aliyekuwa umbali wa takribani mita 10, na kusababisha kifo” alisema Morcase.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, kijana mmoja aitwaye Musa Rashid (19), muokota vyuma chakavu na mkazi wa Masiwa, ndiye aliyekuwa akigonga mfuniko wa mtungi huo kwa lengo la kuufungua, bila kujua hatari iliyokuwepo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Bagamoyo kwa ajili ya taratibu za uchunguzi wa kitabibu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa wito kwa wananchi, hususan waokota na wauzaji wa vyuma chakavu, kuacha mara moja tabia ya kugonga, kukata au kuvunja vifaa vya mitungi ya gesi au mabaki ya vifaa vinavyoweza kusababisha milipuko, ili kuepuka madhara makubwa .