NA JOHN BUKUKU- KATAVI
Wakazi wa Mpanda mkoani Katavi leo wameonyesha hamasa kubwa ya kipekee katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika viwanja vya Azimio.
Maelfu ya wananchi wamejitokeza kwa wingi kuujaza uwanja huo, wakipeperusha bendera za kijani na njano huku wakibeba mabango yenye ujumbe wa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita.
Kauli mbiu isiyo rasmi ya wananchi “Mpanda wameamua kupanda mema kwa Dkt. Samia ili kuvuna maendeleo endelevu” imekuwa kivutio kikubwa katika mkutano huo, ikiashiria imani yao kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea nchini.
Wananchi hao wameeleza kuwa wamethibitishiwa na kazi kubwa iliyotekelezwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji na umeme vijijini, ambayo imechochea uchumi na kupunguza changamoto za kijamii.
“Tumeona mabadiliko makubwa kipindi hiki. Mama Samia ni kiongozi mwenye maono, upendo na utu. Ndiyo maana tumeamua kumpa kura zote za ndiyo tarehe 29 Oktoba,” alisema mmoja wa wananchi katika mkutano huo.
Aidha, wananchi wa Mpanda wameahidi kumuunga mkono Dkt. Samia pamoja na wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani, wakisema hilo ndilo litakalohakikisha kazi inaendelea bila vikwazo.
“Tunataka kazi iendelee, isiwe na makando kando. Mafiga matatu lazima yasimame pamoja – Rais, Mbunge na Diwani wote kutoka CCM,” walisema kwa kauli moja wananchi waliokuwa wakiimba nyimbo za hamasa uwanjani hapo.
Kauli nyingine iliyojitokeza kwa nguvu ni “Mpanda wanapanda na Mama mpaka 2030,” ikionyesha dhamira ya wananchi kuendelea kumuunga mkono katika safari ya maendeleo endelevu.