NA JOHN BUKUKU – KATAVI
Kuna ule usemi usemao “nyota njema huonekana asubuhi”, na ndivyo tunavyoweza kusema baada ya kundi kubwa la ndege wa angani kuonekana likiruka wakati mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Azimio mjini Mpanda, mkoani Katavi.
Tukio hilo lilionekana kama ishara ya namna mgombea huyo anavyokubalika na wananchi wa makundi mbalimbali, ikiwemo hata ndege waliokuwa wakiruka angani kwa furaha baada ya kiongozi huyo kuwasili mkoani humo kuwaomba wananchi wampe ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Samia aliwashukuru wananchi wa Katavi kwa mapokezi makubwa, yenye bashasha na shamrashamra, huku akieleza kuwa alipowasili uwanjani kulikuwa na kundi kubwa la ndege waliokuwa wakiruka juu kana kwamba wanawashangilia viongozi mbalimbali waliokuwepo, wakiwemo Jumaa Aweso na Mwigulu Nchemba.
Alisema kuwa mikoa ya Katavi na Rukwa imekuwa na uwekezaji mkubwa uliotokana na juhudi za Serikali ya CCM katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 iliyopita, ambapo imefunguka kiuchumi kupitia njia mbalimbali ikiwemo barabara, reli, usafiri wa majini pamoja na kuimarika kwa huduma za kijamii ambazo zimewawezesha wananchi kiuchumi.
Dkt. Samia alibainisha kuwa katika mkoa wa Katavi miradi mingi imekamilika, ikiwemo kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Aidha, alitaja kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Karema katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Zambia.
Alisema ujenzi huo umegharimu fedha nyingi na unaenda sambamba na ujenzi wa meli nne za mizigo katika Ziwa Tanganyika. Pia aliongeza kuwa kazi inaendelea vizuri na kwamba kuelekea mwaka 2030, serikali inalenga kuona biashara kubwa kati ya Tanzania na DRC ikipita kupitia Bandari ya Karema.
Kwa upande wa reli, alisema usanifu wa maboresho ya reli ya Kaliua–Mpanda yenye urefu wa kilomita 210 umekamilika, na ukarabati huo utapunguza muda wa safari kutoka masaa 7 hadi 8 hadi kufikia masaa 2 au 3 pekee.
Kuhusu barabara, Dkt. Samia alisema kazi zinaendelea vizuri, ikiwemo barabara muhimu inayounganisha Wilaya ya Tanganyika (Katavi) na Wilaya ya Uvinza (Kigoma), inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda–Sikonge–Mishambu–Uvinza hadi Kanyazi yenye urefu wa kilomita 250.4. Ujenzi huo umefikia asilimia 15.7, na unatekelezwa kwa vipande vinne. Aliahidi kuwa serikali itaongeza kasi ya kukamilisha mradi huo muhimu.
Vilevile, aliahidi kuwa barabara ya Mpanda hadi Kaliua, ambayo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa huo, ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali, sambamba na barabara nyingine zilizoorodheshwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami na changarawe.
Aliongeza kuwa serikali pia itakamilisha ujenzi wa madaraja katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi. Akasema katika miaka mitano ijayo, madaraja hayo yatatekelezwa kwa vitendo.
Dkt. Samia alitaja pia mpango wa kujenga Daraja la Kagese na Daraja la Igwala, pamoja na madaraja madogo ya mawe, ili kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya usafiri inayosababishwa na ukosefu wa madaraja hayo.
Kuhusu wananchi 243 waliopisha ujenzi wa miradi ya barabara ya Mpanda–Sikonge iliyokamilika mwaka 2021, na wananchi 830 waliopisha ujenzi wa barabara ya Mpanda–Sigadike tangu mwaka 2012/2013, Dkt. Samia aliahidi kuielekeza Wizara ya Ujenzi kufanya upembuzi wa madai hayo ili walio na haki halali waweze kulipwa fidia zao.
Akizungumzia usafiri wa anga, alisema serikali imeimarisha huduma hiyo kwa kuboresha uwanja wa ndege wa Mpanda, ikiwemo ujenzi wa jengo la abiria. Aliongeza kuwa kwa sasa usafiri wa anga kutoka Mpanda (Katavi) hadi Dar es Salaam umeboreshwa na unafanyika kwa ufanisi mkubwa.