NA JOHN BUKUKU, KATAVI NA RUKWA
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea leo na kampeni zake katika mikoa ya Katavi na Rukwa, ambapo anatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika maeneo ya Mpanda Mjini, Kibaoni na Namanyere (Nkasi).
Mikutano hiyo ni mwendelezo wa kampeni zake za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, baada ya awali kufanya mikutano mikubwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo alisisitiza umuhimu wa umoja, ushirikiano na amani kama nguzo kuu za maendeleo ya taifa.
Katika hotuba zake zilizopita, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza katika sekta za kilimo, elimu, afya, maji, miundombinu na nishati, ili kufungua fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi hasa wa vijijini.
“Tumejipanga kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi. Tumejenga barabara, vituo vya afya, shule na tunaleta umeme vijijini ili kuchochea maendeleo. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya amani na umoja tulionao,” alisema hivi karibuni Dkt. Samia katika moja ya mikutano yake.
Aidha, Dkt. Samia amekuwa akihimiza wananchi kujiandaa kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani na utulivu.
“Nawaomba Watanzania wote mjitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29. Baada ya kupiga kura, rudi nyumbani mkapumzike kwa amani mkisubiri matokeo, kwa sababu nchi yetu ipo salama na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu. Hakuna sababu ya hofu wala vurugu,” alisema Dkt. Samia.
Wananchi wa Katavi na Rukwa wameelezea hamasa kubwa kwa ziara ya mgombea huyo wa urais, wakisema wanatarajia kumpokea kwa shangwe na kumsikiliza kuhusu vipaumbele vya serikali ijayo katika kuimarisha huduma za jamii na kukuza uchumi wa wananchi.