TMDA inautaarifu umma kuwa, imefanikiwa kuendelea kushikilia hadhi ya Kiwango cha Tatu cha Ukomavu (WHO Maturity Level 3) wa Mfumo wa Udhibiti wa Dawa na Chanjo kufuatia tathmini ya kina iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2023.
TMDA inajivunia hatua hii ya mafanikio kwa kuwa inadhihirisha umahiri wa kazi za udhibiti kwa uwazi, weledi na kwa kufuata viwango vinavyokubalika kimataifa katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za afya.
Toka mwaka 2018, Tanzania kupitia TMDA iliweka historia ya kuwa Mamlaka ya kwanza ya udhibiti wa bidhaa za afya barani Afrika kufikia hatua hii ya WHO Maturity level 3 (WHO ML3). Kushikilia hadhi hii baada ya ukaguzi hakiki uliofanyika mwaka 2023, ni ishara ya mifumo endelevu ya udhibiti ambayo inathibitisha uongozi na mchango wake mkubwa katika kulinda afya ya jamii.
Hii ni hatua muhimu kwa afya ya jamii, ikijumuisha, uhakika wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa na chanjo, ulinzi dhidi ya dawa duni au bandia, na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya kama milipuko ya magonjwa. Aidha, hatua hii ni uthibitisho wa jitihada endelevu za TMDA katika kuimarisha mifumo ya udhibiti, na inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri kimataifa, hususan katika ushiriki wa programu za pamoja za udhibiti, kuongeza fursa za masoko ya kikanda na kimataifa, pamoja na kuvutia wawekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba.
TMDA inawaalika kusherehekea mafanikio haya kama nchi na inatambua mchango wa washirika wa maendeleo, wadau mbalimbali, wataalamu wa afya, na wananchi kwa ujumla katika kulinda afya ya jamii.