Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo (wa kwanza kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore wakitembelea mabanda kabla ya kufungua mkutano na wamiliki wa viwanda na waajiri uliofanyika leo Oktoba 17, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
…………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi yanatoa nguvukazi yenye ujuzi, ubunifu na umahiri wa kukidhi mahitaji ya ajira na maendeleo ya viwanda kwa sasa na siku zijazo.
Akizungumza leo Oktoba 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa elimu ya ufundi, wamiliki wa viwanda na waajiri, ulioratibiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Nombo amesema kuwa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) umejikita katika kujenga mfumo wa elimu unaochochea ubunifu, tija na ushindani katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Amebainisha kuwa moja ya malengo ya sera hiyo ni kuinua ubora wa elimu na mafunzo, kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta binafsi, pamoja na kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa sawa ya kujifunza na kujiendeleza kulingana na mahitaji ya uchumi wa sasa.
“VETA imeendelea kuboresha mitaala, miundombinu na mbinu za ufundishaji ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika mazingira halisi ya kazi,” amesema Profesa Nombo.
Kwa mujibu wa taarifa alizozitoa, Tanzania ina zaidi ya vyuo 900 vya ufundi stadi, ambapo VETA inaendesha vyuo 80 vinavyowahudumia zaidi ya wanafunzi 300,000 kila mwaka.
Pia, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 64 katika wilaya mbalimbali pamoja na chuo kikuu cha mkoa wa Songwe.
Profesa Nombo ameongeza kuwa ifikapo mwaka 2026, VETA itakuwa na vyuo 145 katika wilaya zote nchini, jambo litakaloongeza upatikanaji wa elimu ya ufundi na kuchochea uzalishaji wenye tija kwa jamii.
Aidha, amepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya VETA, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, akisisitiza kuwa mashirikiano hayo yamekuwa kichoche.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, amesema kuwa ushiriki wa wadau katika mikutano ya taasisi hiyo ni wa muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu yenye mchango chanya kwa maendeleo ya taifa.
CPA Kasore amesema kuwa VETA itaendelea kuhakikisha inazalisha wahitimu wenye sifa stahiki na uwezo wa kufanya kazi katika viwanda na makampuni mbalimbali nchini, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Ili tuweze kusonga mbele, tumeanza kwa kupitia mitaala yetu. Tunakutana na wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kujadiliana nao, na baada ya kukamilisha hatua hiyo, tunakwenda kurasimisha mitaala hiyo,” amesema CPA Kasore.