Katibu wa Idara ya Siasa Mafunzo na Uenezi mkoa wa Rukwa Godfrey Mwanisawa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Sumbawanga.
………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Katibu wa Idara ya Siasa Mafunzo na Uenezi mkoa wa Rukwa Godfrey Mwanisawa ametangaza ujio wa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha mapinduzi ( CCM) Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Oktoba 17,2025 Mwanisawa amesema mgombea urais kupitia chama cha mapinduzi Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwasili Mkoani Rukwa 18,2025 akitokea mkoani Katavi na anatarajia kufanya mkutano wa kampeni majira ya saa saba mchana wilayani Nkasi katika mji wa Namanyere katika uwanja wa sabasaba ambapo atahutubia na kuomba kura na kuwaombea wagombea udiwani na ubunge.
Mwanisawa ameongeza kuwa siku ya Oktoba 19,2025 majira ya asubuhi Dkt Samia Suluhu Hassan atahutubia mkutano mkubwa katika uwanja wa shule ya sekondari Kizwite.
“Tunarajia mkutano huo kuhudhuriwa na wananchi, viongozi,wanachama,wakereketwa ,wafurukutwa wapenzi wa chama cha mapinduzi,wapenda maendeleo na makundi mbalimbali kutoka wilaya zote nne za mkoa wa Rukwa.” Amesema Mwanisawa
Aidha Dkt Samia akiwa Mkoani Rukwa atapata nafasi ya kuwakabidhi ilani wabunge na madiwani na ataomba kura na kuwaombea wagombea hao.
Mkoa wa Rukwa una jumla ya kata 97 na chama cha mapinduzi kimewasimamisha wagombea udiwani katika kata zote na majimbo matano 5 wamesimama wagombea wa ubunge kupitia chama hicho.
Dkt Samia ataelezea mafanikio yaliyopatikana ya ilani ya 2020/2025 na atanadi ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030,na kubainisha vipaumbele katika ilani hiyo,pamoja na mambo mengine mbalimbali yatakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwanisawa ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kuwachagua viongozi waliogombea kutoka chama cha mapinduzi ifikapo oktoba 29 ,2025.
Sambamba na hilo pia Mwanisawa amesema vyombo vya dola mkoani hapo pamoja na tume huru ya uchaguzi imewahakikishia kuwa uchaguzi utakuwa huru na amani.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Neema Majaliwa kutoka mtaa wa jangwani amesema ujio wa mgombea wa urais ni fursa kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa hasa wajasiliamali ambao watauza chakula na vinywaji.
“Ujio wa mgombea wa urais ni fursa kwetu
nitauza vinywaji na wengine chakula lakini pia wenye nyumba za kulala wageni tayari wamepokea wageni kutoka maeneo mbalimbali tunamsubiria na tunamkaribisha Rukwa.” Amesema Majaliwa.