Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Ako Tanzania Community Support limesaidia jamii ya wakazi wa kijiji cha Losoito kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa kujenga madarasa matatu shule ya msingi Emishiye, kumalizia zahanati ya kijiji na kuwawezesha wanawake kupitia mradi wa lishe wa kilimo cha mbogamboga.
Mkurugenzi wa shirika la Ako Tanzania Community support, Hilda Kimathi ameeleza kwamba wamesaidia jamii ya eneo hilo kwa kujenga madarasa, kumalizia zahanati na kuwezesha vikundi vya wanawake wanaolima mboga mboga.
Kimathi amesema walipokea ombi toka Losoito na wakajenga chumba cha wanafunzi wa darasa la kwanza na sasa wanajenga madarasa mengine mawili ambayo yatazinduliwa hivi karibuni yakikamilika.
“Tunawashukuru partners wetu, Tansania hilfe, Ingrid Miertsch na Hubert kupitia shirika la Aktionskreis Ostafrika e. V. Germany kwa kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo matatu ya shule ya Emishiye,” amesema Kimathi.
Amesema watoto wachekechea walikua wanakaa chini, watoto wa darasa la kwanza na la pili walikua wanasomea katika chumba cha darasa moja, sasa hivi wanajenga madarasa mengine mawili mapya.
“Kwa upande wa afya tulimalizia ujenzi wa zahanati, choo na jengo la mama na mtoto ila tunaiomba serikali iwapatie daktari ili aweze kutibu watu kwani hakuna tabibu,” amesema Kimathi.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwao katika kufanikisha miradi mbalimbali wanayofanya kwa jamii.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Emishiye, Loishiye Laizer amewashukuru Ako Tanzania Community support kwa kusaidia kuongeza ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.
Mwalimu Laizer amesema jitihada za Ako zimeonekana kwani shule ilikuwa na wakati mgumu ila waliwapatia vifaa vya kufundishia Ipad wanafunzi wa chekechea wa shule hiyo.
“Tulikuwa na wakati mgumu ila Ako Tanzania wametujengea madarasa hayo, pia wametupatia madawati 20 meza ya walimu na viti, kwa kweli wameiunga mkono serikali katika kusaidia jamii,” amesema mwalimu Laizer.
Mwenyekiti wa kijiji cha Losoito, Samson Sakwei ameeleza kuwa Ako Tanzania imekuwa msaada kwao kwani maendeleo waliyofanya katika sekta mbalimbali ni makubwa mno.
Sakwei ameeleza kuwa pamoja na elimu, wamemalizia zahanati ya kijiji na choo cha kisasa na kufanikisha mradi wa lishe wa kikundi cha wanawake kwa kilimo cha mbogamboga.
Mkazi wa kijiji cha Losoito, Tipiliti Kuya amelishukuru shirika la Ako lkwa kuwajengea chumba cha darasa la kwanza na sasa wanajenga madarasa mengine mawili mapya kwa wanafunzi wa chekechea.
“Awali watoto walikuwa wanasomea chini ya miti na kugaragara kwenye udongo ila kwa msaada huu wa Ako Tanzania wa ujenzi wa madarasa hayo watasoma katika mazingira mazuri,” amesema.