Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 17, 2025 jijini Dar es Salaam.
…………..
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo ni mikoa ya Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma, na kusini mwa Morogoro, kwa kipindi cha miezi ya Novemba 2025 hadi Aprili 2026.
Akitoa utabiri huo kwa vyombo mbalimbali vya habari leo, Oktoba 17, 2025, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, na Dodoma.
Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
“Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma, na kusambaa katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba 2025. Zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi,” alifafanua Dkt. Chang’a.
Aliongeza kuwa, “Msimu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi, japokuwa kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili 2026) kinatarajiwa kuwa na ongezeko la mvua ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba 2025 – Januari 2026).”
Akieleza athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema mvua za chini ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi zinaweza kusababisha upungufu wa unyevu wa udongo, jambo ambalo linaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mazao na hivyo kupunguza mavuno, hususan kwa mazao yanayotegeamea mvua.
Aidha, kupungua kwa kina cha maji kwenye mabwawa na mtiririko wa maji kwenye mito kunaweza kutokea, hali ambayo inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali. Vilevile, upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo unatarajiwa kuathirika.