NA JOHN BUKUKU- BUKOBA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali imejipanga kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 6 hadi 10 ifikapo mwaka 2030 kupitia kilimo biashara, mikopo, mafunzo na ruzuku kwa wakulima.
Amesema mkakati huo unalenga kuongeza tija, ajira na kipato cha wananchi vijijini, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa, pembejeo bora na mbegu zenye ubora wa hali ya juu. Ameongeza kuwa katika sekta ya uvuvi, Serikali itawawezesha wavuvi kufanya uvuvi wa kisasa kwa mikopo, nyenzo na mafunzo, pamoja na kufuga samaki kwenye vizimba kupitia mradi maalum wa “Bibi Titi – Jenga Kesho Iliyo Bora.”
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuongeza thamani ya mifugo kupitia kampeni za chanjo, utambuzi wa mifugo na ujenzi wa machinjio ya kisasa ili kutimiza viwango vya kimataifa na kuongeza mauzo ya nje ya mazao ya mifugo.
Pamoja na maendeleo hayo katika sekta ya uzalishaji, Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo ndani na nje ya Ilani ya CCM katika sekta mbalimbali, hatua iliyochangia maendeleo makubwa nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza Oktoba 16, 2025, na wananchi na wakazi wa Bukoba mkoani Kagera, Dkt. Samia amesema kuwa tangu alipozuru mkoa huo mwaka 2022 kama Rais, alitoa maelekezo kadhaa kuhusu namna ya kuinua uchumi wa Kagera na kupunguza umasikini, ambapo kamati iliyoongozwa na Dkt. Bashiru Ally, Mama Tibaijuka na wengine iliunda mpango kazi unaotekelezwa kwa sasa.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeboresha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali za rufaa, zikiwemo huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Amesema idadi ya wagonjwa waliotibiwa imeongezeka kutoka 128,305 mwaka 2021 hadi 478,002 mwaka 2025, jambo lililopunguza utegemezi wa hospitali za Bugando na Muhimbili.
Dkt. Samia amesema katika miaka mitano ijayo Serikali itazingatia zaidi kuongeza ubora wa huduma za afya sambamba na utekelezaji wa Sera ya Bima ya Afya kwa Wote, ili kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu bora bila mzigo wa kifedha kwa familia. Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaanza kuajiri wataalamu 5,000 wa sekta ya afya ndani ya siku 100 za kwanza za utawala wake endapo watapewa ridhaa.
Katika sekta ya elimu, Dkt. Samia amesema Serikali imejenga shule nyingi za msingi na sekondari nchini, huku elimu bila ada ikiendelea kutekelezwa kwa mafanikio. Ameongeza kuwa mkoani Kagera zimejengwa shule tatu za amali, shule ya sayansi ya wasichana pamoja na vyuo vitano vya VETA ikiwemo Chuo cha Mkoa cha Burugo. Amesema pia ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani humo umefikia asilimia 70.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuongeza mabweni kwenye shule za sekondari hasa maeneo ya visiwani ili kuwawezesha wanafunzi kusoma bila changamoto za usafiri. Pia Serikali itaendelea kutunisha mfuko wa elimu ya juu ili wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wapate mikopo bila usumbufu.
Aidha, katika sekta ya nishati, Dkt. Samia amesema Serikali imetekeleza agizo la Ilani la kufikisha umeme vijijini kote nchini na sasa inajipanga kukamilisha vitongoji vyote ifikapo mwaka 2030. Amelitaja pia mkoa wa Kagera kuwa na miradi mikubwa ya kuzalisha umeme wa maji yenye jumla ya megawati 208 ikiwemo Rusumo, Ngara, Murongo-Kikagati na Kakonko.
Amesema miradi hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika “twenty four seven” na kuchochea uanzishaji wa kongani za viwanda pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Katika sekta ya maji, Dkt. Samia amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama karibu na makazi yake, huku akibainisha kuwa kazi hiyo ipo katika hatua nzuri.
Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, Dkt. Samia amesema Serikali imepanga kujenga soko kubwa la wamachinga (Machinga Complex) katika eneo la Misheni mjini Bukoba kwa gharama ya Shilingi bilioni 10.
Pia, amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kwamba kadri uchumi unavyokua ndivyo kiasi cha fedha kinavyoongezeka.
Aidha, Dkt. Samia amewataka wananchi wa Kagera na Watanzania kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Amesema kuwa, “Tuendelee kufanya kazi, tulime kwa wingi, tuuze kwa wingi, Halmashauri zikusanye zaidi ili fedha hizi ziwanufaishe wananchi,” amesema Dkt. Samia.