NA JOHN BUKUKU – BUKOBA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema kuwa Mkoa wa Kagera ni kumbukumbu hai ya ushujaa wa Watanzania kutokana na historia yake iliyojaa majaribu, mapambano na uvumilivu mkubwa wa wananchi wake.
Amesema kuwa Kagera ni mahali ambapo historia, maumivu na matumaini vimekutana na kujenga taifa lenye ushupavu na uvumilivu. Ameeleza kuwa katika historia ya taifa letu, mkoa huo umebeba heshima kubwa, ikiwemo vita dhidi ya Nduli Idi Amin Dada, ambako Watanzania walilinda mipaka kwa ujasiri na kulinda heshima ya taifa.
Aidha, Dkt. Migiro amebainisha kuwa licha ya changamoto mbalimbali kama vile vita, janga la UKIMWI na athari za mabadiliko ya tabianchi, wananchi wa Kagera wameendelea kuonesha uthabiti na kujituma katika kujenga upya maisha yao na taifa kwa ujumla.
Amebainisha kuwa mkoa wa Kagera umeendelea kuwa mfano wa maendeleo na ustahimilivu, akisema kwamba juhudi za Dkt. Samia zimeimarisha uchumi, miundombinu na ustawi wa jamii.
Amesema kuwa Bukoba ya leo ni taswira ya mafanikio ya falsafa ya 4R ya Dkt. Samia, akieleza kuwa ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, pamoja na miradi ya barabara na bandari ni ushahidi wa utekelezaji wa falsafa hiyo.
Aidha, Dkt. Migiro amebainisha kuwa mageuzi katika elimu ni sehemu muhimu ya falsafa hiyo, na kwamba wananchi wa Kagera wameshuhudia maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia.
Amesema kuwa maridhiano yameonekana wazi kupitia umoja wa wananchi wa makundi yote waliokusanyika kwa pamoja, akisisitiza kuwa hata wale walio nje ya Chama Cha Mapinduzi wamevutiwa na jitihada za Rais Samia katika kuleta maendeleo na mageuzi ya kweli kwa taifa.
Dkt. Migiro amebainisha kuwa wananchi wa Kagera wanampokea mgombea urais wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama kiongozi aliyeahidi na ametimiza, aliyeahidi na ametenda.
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia amesimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, na sasa anabeba Ilani ya 2025–2030 sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050.