Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mh Jaffar Haniu ametoa wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Rungwe na Busekelo kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika siku ya tarehe 29, Oktoba mwaka huu 2025.
Uchaguzi mkuu utahusisha Wananchi Kumchagua Rais, wabunge pamoja na Madiwani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 16 Oktoba 2025 Mh Haniu amewasihi wananchi wasikubali kurubuniwa na watu wasio na nia njema kama kuombwa watoe kadi ya kupigia kura, kushiriki maandamano au vurugu zozote kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Mh Haniu ambaye pia ni Mwenyekiti wa ulinzi na usalama wilaya ya Rugwe ameapa kulinda na kusimamia amani na utulivu huku akiwasihi wananchi kutochezea Amani iliyopo kwani kufanya hivyo itadhorotesha shughuli za maendeleo na hata kushindwa kushiriki katika sehemu za ibada.
” Rungwe ni Salama, Itakua salama wakati wa uchaguzi na baada ya Uchaguzi” Ameongeza Mh Haniu
Aidha amewaomba wasimamizi wa uchaguzi kutoa kipao mbele kwa akina mama wajawazito, Wazee, wanaonyonyesha pamoja na walemavu siku ya upigaji wa kura.
Pia amewasihi wananchi kutovaa sare ya chama chochote cha siasa siku ya uchaguzi na pindi watakapomaliza kupiga kura warejee katika makazi yao au shuhuli zao za uzalishaji mali na kusubiri matokeo kwa amani na utulivu.