NA JOHN BUKUKU- KAYANGA KARAGWE
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amemshukuru Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kuendeleza ujenzi wa Bonde la Mto Ngono, mradi ambao ulikuwa umesalia katika makabrasha ya Mpango wa Maendeleo wa Kwanza wa Nchi. Amesema serikali imeamua kutumia shilingi bilioni 500 kukamilisha ujenzi huo muhimu kwa wananchi wa Kagera.
Bashe aliyasema hayo Oktoba 15, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera , ambapo alieleza kuwa Bonde hilo ni uhai wa wananchi wa wilaya zaidi ya nne mkoani humo.
Alifafanua kuwa wazo la Bonde la Mto Ngono lilibuniwa na Askofu Kibira pamoja na Shehe Katura, likihusisha maeneo kuanzia Bukoba Vijijini hadi Misenyi. Hata hivyo, kwa muda mrefu lilikuwa limebaki katika makabrasha ya mipango ya maendeleo ya awali.
Aidha, alisema wananchi wa Kagera, hasa wa Karagwe na Kyerwa, wanahitaji vituo vya biashara, na kupitia mradi wa ACDP 1 serikali imeweka masoko matatu katika mkoa wa Kagera — moja likiwa Ngara na mawili Kyerwa. Aliongeza kuwa wakandarasi wapo kazini kwa ajili ya kujenga masoko hayo ambayo yalikwama kwa zaidi ya miaka 15.
“Lakini baada ya kuingia madarakani Rais Dkt. Samia , ujenzi huu ambao ulikwama kwa miaka 15 umeanza na wakandarasi wapo site,” alisema Bashe.
Akizungumzia zao la kahawa, Waziri Bashe alisema kahawa inalimwa katika mikoa ya Kagera, Ruvuma na Songwe Mbozi. Alibainisha kuwa mwaka 2021/2022 mapato ya mauzo ya kahawa nje ya nchi yalikuwa dola milioni 111, lakini sasa yamefikia dola milioni 338, mafanikio ambayo amesema yametokana na hatua kubwa zilizochukuliwa na Dkt. Samia katika kipindi cha miaka minne.
“Wananchi wa Kagera na maeneo mengine yanayolima kahawa watakuchagua Oktoba 29 kwa sababu umefufua chama chao cha KDCU hapa Kagera. Uliwakamata wahalifu wote, serikali ikawachukulia hatua. Kulikuwa na watu waliokuwa wakinufaika kwa nguvu za wakulima, walijenga magesti na hoteli. Leo, mwaka huu pekee, chama kimechukua mkopo wa bilioni 25, kimenunua kahawa za wakulima kwa bilioni 32 na kuuza nje kwa bilioni 37,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa chama cha KNCU pia kimenufaika, huku akieleza kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali imepanga kufufua Kiwanda cha TANICA kinachomilikiwa na ushirika, kilichoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Amesema fedha zimetolewa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kubadilisha teknolojia ya kiwanda hicho.
Waziri Bashe alisema wameweka mipango kwamba, endapo Dkt. Samia atachaguliwa, serikali itakifufua kiwanda hicho kurudi katika hadhi yake ya miaka ya 1960 na 1970. Aliongeza kuwa wakulima wanapata miche bure na mbolea kwa ruzuku, na kwamba Kagera imeanza kutumia mbolea za viwandani katika mazao yao.
Hata hivyo, alisema baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Dkt. Samia, walikaa na wakulima na wananchi kuhusu tozo na kufuta tozo zote zisizo na tija. Pia, mfumo wa mauzo ya kahawa ulibadilishwa kwa kupiga marufuku biashara ya utura ambapo mtu alikuwa akinunua mazao kwa bei ya hasara kabla ya mavuno.
Bashe alisema hivi sasa wilaya hizo mbili za Karagwe na Kyerwa zinazalisha kahawa tani 25,000, na bei ya mkulima imepanda hadi wastani wa Sh 5,000 kwa kilo. Alibainisha kuwa mkulima sasa hapangiwi bei na wafanyabiashara wa mtura, huku serikali ikigawa miche bure. Katika kipindi cha miaka minne, serikali imegawa jumla ya miche milioni 20 kwa wakulima bila malipo.
“Hata leo, ukiwauliza wakulima watakuambia wanataka miche zaidi. Kagera sasa wameanza kung’oa migomba mibovu na kupanda kahawa kwa sababu wanajua faida yake. Kwa miaka 10 mkulima anaweza kupata zaidi ya shilingi 10,000 kwa kila mti wa kahawa, jambo linaloonyesha mabadiliko makubwa uliyoyafanya,” alisema.
Pia alimshukuru Dkt. Samia kwa mpango wake wa kufufua Kituo cha Utafiti cha Maruku ambacho kilikuwa kimekufa kabisa. Alisema serikali imetoa fedha kwa ajili ya kukijenga upya kituo hicho, kitakachosaidia kuzalisha miche bora ya migomba na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Kagera.