Na Silivia Amandius.
Kagera.
Baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi wameelezwa kuwa chanzo cha kueneza propaganda zinazolenga kuwakatisha tamaa Watanzania walioko nyumbani kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao. Ndg. Allawi amesema hatua hiyo ni hatari kwa mustakabali wa taifa kwani inalenga kudhoofisha misingi ya demokrasia na kuathiri maendeleo ya nchi. Amehimiza Watanzania wanaoishi nje ya mipaka kuwa mabalozi wa maendeleo na si chanzo cha migawanyiko ya kisiasa, akisisitiza kuwa kupiga kura ni haki na wajibu wa kila raia.
Ameeleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya kisiasa kupitia sanduku la kura. Kwa mujibu wake, mataifa mengine duniani huchukulia kushiriki uchaguzi kama ishara ya uzalendo, hivyo ni muhimu Watanzania kuiga mfano huo kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi.
Aidha, Ndg. Allawi amewataka wananchi kutumia fursa ya uchaguzi kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa kwa kuchagua viongozi wenye dira, uwajibikaji na moyo wa kujali maslahi ya wananchi. Amesisitiza kuwa ni jukumu la jamii kuwaelimisha vijana kuhusu haki yao ya kupiga kura na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Kwa upande mwingine, amezitaka taasisi na mashirika ya kiraia kushirikiana katika kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi. Ameahidi kuwa jumuiya ya Watanzania waishio China itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za kukuza demokrasia na kuimarisha maendeleo ya Tanzania.