Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WANANCHI wa Kijiji cha Lunoro kata ya Kipololo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameanza kunufaika na huduma bora za afya kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa zahanati katika kijiji chao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema,tangu Uhuru kijiji chao hakijawahi kuwa na huduma za afya badala yake walizipata katika Hospitali ya Misheni Litembo na Hospitali ya Wilaya Mbuyula iliyopo Mbinga mjini umbali wa kilometa 25.
Gedfrida Kapinga amesema,kabla ya kujengwa kwa zahanati katika kijiji chao mama wajawazito walibebwa kwenye matenga ili kufikishwa Hospitali Litembo inayopatikana umbali wa kilometa 7 na wapo waliofariki Dunia wakiwa njiani kabla ya kufikika kwenye vituo vya kutolea huduma kutokana na ubovu wa Barabara.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Anakilet Kapinga,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia Halmashauri ya Wilaya Mbinga kukamilisha ujenzi wa zahanati ambayo imekuwa msaada kwa kupata huduma za matibabu karibu na maeneo yao.
Kwa mujibu wa Kapinga,miaka ya nyuma walikuwa wanakwenda kata jirani ya Ngima na wengine Hospitali ya Mkoa Songea kufuata matibabu, lakini baada ya kukamilika zahanati yao wanapata huduma hizo kirahisi tofauti na awali.
“Kipindi cha masika tulilazimika kutembea kati ya kilometa 6 hadi 7 kwenda vijiji vingine kupata matibabu,lakini sasa tunapata huduma hapa kijijini kwetu,tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutusogezea huduma za matibabu”alisema.
Aidha,ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwaongezea watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwani waliopo ni wachache kulingana na idadi ya wananchi wanaofika kupata huduma katika zahanati hiyo.
Sisita Matenga alisema,miaka ya nyuma shida kubwa hasa wanawake wajawazito wanapotaka kujifungua kwani walibebwa kwenye matenga na wengine walibebwa kwenye machela ili kufikishwa Hospitali ya Litembo kwa ajili ya kujifungua.
Alisema baadhi ya akina mama na watoto wadogo walifariki wakiwa njiani kutokana na changamoto kubwa ya Barabara ambayo wakati huo ilikuwa mbovu na hakukuwa na usafiri wa uhakika.
Kwa upande wake Katibu wa afya wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga George Mhina alisema,Halmashauri itaendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo yote ya vijijini na mjini kwa kupeleka watumishi wa kutosha,madawa na vifaa tiba ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora.
Alisema,ujenzi wa zahanati hiyo ulianza kwa nguvu za wananchi wenyewe na baadaye Halmashauri ya Wilaya kupitia mapato yake ya ndani iliwaunga mkono kwa kukamilisha mradi huo ambao umesaidia sana wananchi kupata matibabu.
“Miradi hii ya afya imeanzishwa na wananchi wenyewe,Serikali ilikuja kuwaunga mkono kwa kukamilisha ujenzi wake nataka wananchi watambue kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan iko kazini kwa kuhakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya adui maradhi,ni furaha kuona wananchi walishiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi hii ya afya katika vijiji mbalimbali kabla ya Serikali kutoa fedha za kuiendeleza”alisema Mhina.
Amewataka wananchi,kuhakikisha wanasimamia na kutunza miradi hiyo kwani dhamira ya Serikali kuona miradi yote inayotekelezwa inadumu kwa muda mrefu ili kutatua changamoto za wananchi.