Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD) Bw. Shendu Hamis Mwagalla, akikabidhi cheti cha kutambua mchango wa udhamini kwa Bi. Gemma Kamara, Mkuu wa Idara ya Bei za vifurushi na makundi maalumu ya wteja kutoka Vodacom Tanzania PLC, kama ishara ya kuthamini mchango wa kampuni hiyo katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini. Kupitia udhamini huo, Vodacom imeboresha uwanja wa Don Bosco Oysterbay, kudhamini zawadi za washindi wa kwanza, pili na tatu, na kuendeleza programu za kuwawezesha vijana kupitia michezo. Tukio hilo limefanyika katika hafla ya utoaji tuzo za Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL) 2025, mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.
…………….
Dar es Salaam, 13 Oktoba 2025: Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BDL) waliandaa hafla ya tuzo maalum jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kilele cha msimu wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL) 2025. Hafla hiyo ilikusudia kusherehekea mafanikio ya wachezaji, timu na wadau walioshiriki msimu mzima, huku ikiangazia athari chanya za uwekezaji wa Vodacom katika kukuza michezo na vijana nchini.
Ligi ya mwaka huu ilihusisha jumla ya timu 277, kwa upande wa wanawake na wanaume zilizoshiriki katika mashindano yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay, ambao umekarabatiwa na Vodacom kama sehemu ya dhamira yake ya kukuza vipaji na kuinua ari ya vijana kupitia michezo. Tuzo na zawadi zilitolewa kwa mabingwa wa msimu huu pamoja na wachezaji bora wa kike na wa kiume, waliodhihirisha nidhamu na ubunifu uwanjani.
Akizungumza katika halfa hiyo Mkuu wa Idara ya bei za vifurushi na makundi maalum ya wateja, Gemma Kamara Alisema “Kwa Vodacom, ushirikiano huu na BD ni zaidi ya udhamini wa michezo. Ni njia ya kushirikiana na jamii katika kuwawezesha vijana kutambua uwezo wao. Tumejifunza mengi kupitia ligi hii, kuona vijana wakikua, wakijiamini, na kutumia michezo kama nguzo ya maendeleo binafsi na kijamii. Vodacom itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwawezesha vijana kupitia michezo, elimu, na teknolojia kama nguzo kuu za kuwasaidia kufikia ndoto zao
Kwa upande wake, Mpoki Mwakipake, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa kikapu, aliishukuru Vodacom kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini. “Ushirikiano kati ya BD na Vodacom umeleta mabadiliko makubwa katika mchezo huu. Tumeshuhudia ongezeko la ari, nidhamu na ushindani wa kweli. Ni heshima kubwa kuona vijana wetu wakifikia viwango vya juu zaidi” alisema Mpoki Mwakipale, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa kikapu,
“Moja ya changamoto kubwa tunayokutana nayo kama wachezaji ni ukosefu wa miundombinu bora ya michezo,” alisema Nadia Samir, mchezaji wa Don Bosco Troncatti. “Lakini mwaka huu tumefarijika kuona mabadiliko makubwa uwanja wa Don Bosco umeboreshwa kwa udhamini wa Vodacom, ligi imekuwa ya ushindani zaidi. Tungependa kuona wadhamini wengine wakijitokeza ili kuendelea kuboresha mpira wa kikapu nchini Tanzania.”
Kwa upande wa wanaume, Dar City Basketball Team waliibuka mabingwa baada ya ushindani mkali katika michezo ya fainali dhidi ya wapinzani wao JKT, wakijinyakulia zawadi ya shilingi milioni 10 kutoka Vodacom. Kwa upande wa wanawake, DB Lioness Basketball Team walitawala uwanjani na kutwaa taji la ubingwa wa BDL 2025, nao wakipokea zawadi ya shilingi milioni 10 kama sehemu ya kutambua jitihada na mafanikio yao.
Kupitia miradi kama hii, Vodacom inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa vijana wa Kitanzania ikitumia michezo, elimu na teknolojia kama nyenzo za kujenga kizazi kinachojiamini, chenye dira na matumaini ya kesho iliyo bora.
Hafla ya utoaji tuzo ilihudhuriwa na Vodacom, BD, wadau wa michezo, familia za wachezaji na waandishi wa habari. Usiku huo ulipambwa na muziki, furaha na shangwe za vijana waliotimiza ndoto zao kupitia mchezo wa mpira wa kikapu.