𝘔𝘪𝘳𝘢𝘥𝘪 𝘺𝘢 𝘮𝘢𝘫𝘪, 𝘶𝘮𝘦𝘮𝘦 𝘯𝘢 𝘦𝘭𝘪𝘮𝘶 yaemdelea 𝘫𝘪𝘮𝘣𝘰𝘯𝘪 𝘩𝘶𝘬𝘰 𝘬𝘶𝘱𝘪𝘵𝘪𝘢 𝘪𝘭𝘢𝘯𝘪 𝘺𝘢 𝘊𝘊𝘔
NA JOHN BUKUKU- MULEBA
Mgombea ubunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Adonis Alfred Bitegeko, amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo umeendelea kwa kasi kubwa, kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, serikali imewekeza nguvu kubwa katika sekta za maji, umeme, miundombinu na elimu, hatua ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi wa Muleba Kaskazini.
Aidha, Bitegeko amebainisha kuwa miradi ya maji vijijini imeendelea kupanuka, huku serikali ikihakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia wananchi kwa wakati, jambo linalosaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema kuwa katika sekta ya nishati, kazi ya kuimarisha miundombinu ya umeme katika kata nne za jimbo hilo inaendelea vizuri, hatua inayochochea shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato cha wananchi.
Kuhusu elimu, Bitegeko amesema kuwa ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari umefikia asilimia 50, jambo linaloashiria dhamira ya serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kupunguza changamoto za umbali kwa wanafunzi waishio maeneo ya mbali.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea kushughulikia mgogoro wa muda mrefu wa ardhi unaohusisha vitalu vya Muleba Kaskazini, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi bila migogoro.
Bitegeko ameongeza kuwa wananchi wa Muleba Kaskazini wameendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya CCM kwa vitendo, kwa kutambua kuwa sera na ilani yake zimekuwa chachu kubwa ya maendeleo katika maeneo yote ya jimbo hilo.