NA JOHN BUKUKU- KAGERA
Mgombea ubunge Viti Maalum kupitia kundi la vijana mkoa wa Kagera, Halima Abdallah Bulembo, amesema kuwa yeye pamoja na vijana wenzake wana furaha kubwa kumpokea mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani anaamini maendeleo yote yanayotekelezwa na serikali ni kwa manufaa ya vijana.
Ameyasema hayo Oktoba 15, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutambua nafasi yao katika kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia.
Bulembo amesema kuwa yeye kama kijana, pamoja na vijana wenzake wa Kagera, wanampongeza sana Mama Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo, na wako tayari kumpigia kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha, amebainisha kuwa wananchi wa Kagera wanajihusisha zaidi na zao la kahawa, na kwamba katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta hiyo imepewa kipaumbele kikubwa kutokana na umuhimu wake katika kuinua uchumi wa wananchi na hasa vijana.
Amesema vijana wa Kagera wako tayari kuhakikisha Serikali ya Mama Samia inaendelea kulipa kipaumbele zao hilo kwa vitendo, kwani limekuwa chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwao.
Bulembo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa mipango mingi ya maendeleo inayotekelezwa nchini inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kielimu na kijamii.
“Vijana lazima tuitambue nafasi yetu. Maendeleo yote tunayoyaona — kuanzia elimu, ajira, mikopo, na miundombinu — yote haya yanafanywa kwa ajili yetu. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunachagua CCM ili kazi hii ya Mama Samia iendelee kwa vitendo,” alisema Bulembo.
Aidha, amebainisha kuwa katika nyakati zote za uchaguzi, vijana wengi wamekuwa wakichagua upande sahihi wa maendeleo kwa kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeendelea kuwaletea matumaini na mwelekeo bora wa maisha.