NA JOHN BUKUKU – KAGERA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuendelea na kampeni zake leo mkoani Kagera kwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika maeneo ya Muleba, Kayanga na Kyaka.
Katika mikutano hiyo, Dkt. Samia anatarajiwa kuzungumza na wananchi kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na kueleza dira ya maendeleo ya CCM kwa miaka mitano ijayo.
Aidha, anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kama msingi wa mafanikio ya maendeleo, akibainisha kuwa taifa lenye amani ndilo linaloweza kujenga uchumi imara na kuimarisha ustawi wa wananchi wake.
Dkt. Samia pia anatarajiwa kugusia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kagera, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, sekta ya elimu, afya, maji na umeme vijijini, miradi ambayo imesaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Vilevile, atawahimiza wananchi wa Kagera kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, kupiga kura kwa amani na utulivu, kisha kurejea majumbani kusubiri matokeo kwa subira.
Kampeni za CCM zinaendelea leo katika maeneo hayo ya Mkoa wa Kagera, zikiwa na lengo la kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na wananchi ili kujadili utekelezaji wa sera za maendeleo na mipango ya miaka ijayo.