Muonekano wa Zahanati ya Mahenge kata ya Mahenge Halmashauri ya Wlaya Mbinga Mkoani Ruvuma iliyojengwa na wananchi wa kjiji hicho kwa kushirikiana na Halmashauri tya Wilaya Mbinga.
Zahanati ya Kijiji cha Lugali kata ya Mkumbi kama inavyoonekana.
………….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
HALMASHAURI ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,imeweka Historia kwenye sekta ya afya baada ya kufungua zahanati nane kwa wakati mmoja ili kuondoa adha,kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Katibu wa Afya wa Halmashauri hiyo George Mhina,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizo na kuweka kipaumbele kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na wananchi.
Alisema,kufunguliwa kwa zahanati hizo ni faraja kubwa kwa wananchi ambao walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda vijiji vingine kufuata huduma hizo.
Alisema,katika utekelezaji wa miradi hiyo wananchi wameitikia vizuri mpango wa kuboresha afya ya msingi(MAM)kwa kujenga zahanati kila Kijiji lakini kutokana na changamoto ya fedha walishindwa kukamilisha kwa wakati.
“Sisi kama Serikali baada ya kuona na kutambua nguvu kubwa za wananchi tulijipanga kwa kuhakikisha zahanati hizo zinakamilika kwa kuwapelekea fedha ili kutoa huduma kwa wananchi”alisema Mhina.
Aidha alisema,kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 Halmashauri ya Wilaya Mbinga imefungua vituo mbalimbali 23 ikiwemo Hospitali ya Halmashauri 1,vituo vya afya 4 na zahanati 17 ambazo zimekamilika,kupeleka watumishi,daw ana vifaa tiba ili kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema, katika utekelezaji wa miradi hiyo Halmashauri ya Wilaya Mbinga imetumia zaidi ya Sh.bilioni 1.3 kukamilisha zahanati hizo na kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wanatarajia kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya 17 ambazo zitagharimu Sh.bilioni 1.3.
“Kama mambo yakiende vizuri tunaamini kabla ya mwezi Juni 2026 zahanati zote zitakamilika na kufunguliwa,kipekee tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa karibu na ubora na vifaa tiba na watumishi wanapatikana kwa ajili ya kuwahudumia wananchi”alisema Mhina.
“Tunampongeza Mkurugenzi wetuMtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Joseph Kashushura,kwa kutoa fedha za miradi hiyo kwani angeweza kuzipeleka sehemu nyingine,lakini kwa kutambua changamoto za huduma ya afya ameamua kuzipeleka fedha hizo kwenye sekta ya afya ili wananchi wapate huduma bora.
Tabibu wa zahanati ya Mahenge Bahati Kiponda,ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha katika Kijiji hicho kunakuwa na huduma bora za afya ili wananchi waweze kuondokana na changamoto kubwa ya afya na kushiriki kazi za uzalishaji mali.
Alisema,tangu zahanati hiyo ifunguliwe wananchi wanakwenda kupata huduma na kuondokana na kero iliyokuwepo kwa muda mrefu kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.
Mkazi wa Kijiji cha Mahenge Renata Komba alisema,kabla ya kukamilika kwa zahanati hiyo walikwenda Hositali ya Litembo inayopatikana umbali wa kilometa 5 kwenda kupata matibabu,hata hivyo akina mama wajawazito na watoto walishindwa kufika kwa wakati hali iliyosababisha wengine kupoteza maisha wakiwa njiani.
Bruno Komba alisema,zahanati hiyo ni mkombozi mkubwa kwao kwani awali walikwenda hadi Kijiji cha Litembo na Hospitali ya Wilaya Mbuyula iliyopo Mbinga mjini kwa ajili ya kufuata huduma za matibabu ambako walikuwa wanatumia gharama kubwa zikiwemo za usafi na matibabu.
“Zahanati ya Mahenge ni mkombozi mkubwa sana kwetu,kwani licha ya kuhudumia kijiji cha Mahenge lakini hata wananchi wa vijiji vingine vya jirani wanategemea kupata huduma hapa,tunaishukuru Halmashauri ya Wilaya Mbinga kutuunga mkono katika ukamilishaji wake kwani sisi ndiyo tuliyoanzisha ujenzi wake”alisema Komba.
Komba,ameiomba Serikali kuifanya zahanati hiyo kuwa kituo ha afya kwa sababu zahanati hiyo kwa sasa inahudumia watu wengi ambao wanahitaji kupata huduma kubwa zaidi ikiwemo ya upasuaji ambayo kwa sasa haipatikani
Muonekano wa Zahanati ya Mahenge kata ya Mahenge Halmashauri ya Wlaya Mbinga Mkoani Ruvuma iliyojengwa na wananchi wa kjiji hicho kwa kushirikiana na Halmashauri tya Wilaya Mbinga.