NA JOHN BUKUKU- MULEBA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa serikali italeta boti maalum mbili za ambulance kwa ajili ya kata za Goziba na Bumbile, wilayani Muleba, ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za dharura kwa wakati.
Akizungumza Oktoba 15, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Muleba Kaskazini mkoani Kagera, Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto ya usafiri wa wagonjwa, hasa katika maeneo ya visiwani ambako wananchi wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa kusafirisha wagonjwa kwenda hospitalini kwa haraka.
Amesema serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wa maeneo yote ya vijijini na visiwani wanapata huduma bora za afya, ikiwemo upatikanaji wa usafiri wa majini wa uhakika kwa wagonjwa.
Dkt. Samia amesema sambamba na kuleta boti hizo, serikali pia itajenga gati mbili katika vijiji vya Kitua na Bruno, ambazo zitarahisisha shughuli za upakiaji na upakuaji wa abiria na mizigo, na hivyo kuboresha huduma za usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya shilingi bilioni 39.35, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika vijiji vyote.
Aidha, amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha huduma za kijamii kama afya, elimu na miundombinu ya nishati zinaboreshwa zaidi, huku akisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwekeza katika miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa Muleba na mikoa mingine nchini.
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi Ilani ya Uchaguzi baadhi ya wagombea Ubunge wa Majimbo mbalimbali Mkoa wa Kagera mara baada ya kuwahutubia wananchi wa Muleba mkoani humo tarehe 15 Oktoba, 2025.