Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Beijing, China.
Tanzania kupitia Viongozi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeshiriki katika Mkutano wa Viongozi wa Dunia Kuhusu Wanawake “Global Leaders’ Meeting on Women” uliofanyika Beijing, nchini China.
Akizungumza tarehe 13 Oktoba 2025 kando ya Mkutano huo Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao ambaye ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania amesema wameshiriki Mkutano huo kwa lengo la kujifunza na kutoa uzoefu wa namna bora ya kufikia Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa wanawake.
“Tumejadili mafanikio na changamoto zinazokabili nchi mbalimbali katika kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake tangu kuwekwa kwa maazimio ya malengo ya Beijing mwaka 1995” amesema Vickness.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Wanawake kutoka Wizara hiyo Juliana Kibonde amesema mkutano ulioandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu China chini ya Umoja wa Wanawake wa Chama Tawala “All-China Women’s Federation” kwa kushirikiana na U.N Women umekuwa na mchango mkubwa hasa kwa nchi mbalimbali kujifunza na kueleza mafaniko na changamoto zao katika kufikia Usawa wa Kijinsia katika Mataifa yao.
“Mkutano ulikuwa na lengo la kusherehekea na kufanya tathmini ya miaka 30 ya Mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 hapa Beijing na sasa ni miaka 30 tukiwa tunasherekea mafanikio ya utekelezaji wa malengo 12 ya Mkutano huo ambayo kila nchi ilichagua kutekeleza na kuangalia changamoto zilizobaki ili kuweza kutatua na kuzifanyia kazi ili kuwa na Dunia yenye Usawa wa jinsia na Uwezeshaji wa wanawake” amesisitiza Juliana.
Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping huku ukihudhuliwa na Viongozi wakuu wa nchi na Serikali, Mawaziri pamoja na Mabalozi kutoka takribani nchi zaidi 110, Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa huku zaidi ya washiriki 800 wakihudhuria mkutano huo.
Mkutano huo uliongozwa na kaulimbiu isemayo “Mustakabali wa Pamoja: Mchakato Mpya na Uliorahishwa kwa Maendeleo Jumuishi ya Wanawake”.