Mkuu wa mkoa wa Arusha, Amos Makala akizungumza kwenye hafla hiyo jijini Arusha leo.
Mwenezi wa Chama cha Wanaume Wazee Tanzania (CCWWT) ,Sabas Kisakeni akizungumza kwenye half hiyo jijini Arusha.
……………….
Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Amos Makala amewaasa vijana kuendelea kutunza amani na utulivu wa nchi yetu hasa wanapoelekea kwenye kipindi cha uchaguzi na kuepuka vitendo vya vurugu ,fujo,na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuchochea migogoro.
Aidha amewataka vijana hao kutohamasika na mihemko ya mitandaoni inayoweza kuchochea uvunjifu wa amani katika nchi yetu badala yake wahakikishe wanahamasisha amani na utulivu kama ambavyo wazee wetu wamekuwa wakifanya.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika matembezi ya amani na mshikamano wa Taifa katika kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere yaliyoanzia katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Arusha hadi viwanja vya Makumbusho ya azimio la Arusha.
Amesema kuwa ,vijana wana wajibu na nafasi kubwa katika kuhakikisha wanatunza amani ya nchi yetu ili kuhakikisha inabaki salama endapo wataondokana na matumizi mabaya ya mitandaoni inayochochea migogoro mbalimbali.
“Vijana tunatakiwa tuige mfano kwa wazee wetu kama ambavyo wanafanya katika kuhakikisha wanahubiri amani na utulivu kila mahali kwani hadi kufikia hapa wameona mambo mengi sana ambayo na sisi tunapaswa kujifunza kutoka kwao.”amesema Makala.
Kwa upande wake Mwenezi wa Chama cha Wanaume Wazee Tanzania (CCWWT) ,Sabas Kisakeni amesema kuwa matembezi hayo yamewashirikisha wazee mkoa wa Arusha kutoka makundi mbalimbali yakiwemo baraza la wazee,chama cha wazee wanaume Tanzania,umoja wa wazee mkoa na wazee wa mila kwa ujumla.
Kisakeni amesema kuwa, lengo la matembezi hayo kwa hiari ni kuimarisha afya zao,kutoa elimu kwa jamii juu ya mambo mbalimbali ikiwemo amani na mshikamano na kuhamasisha jamii nzima kuhakikisha inashiriki kwenye zoezi la uchaguzi mwezi huu.
“Tunaishukuru sana awamu ya sita inayoongozwa na mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya kwa wazee,kuhakikisha pensheni ya wastaafu inapatikana kwa wakati na imeendelea kuboreshwa ,kuhakikisha wazee wanaendelea kushirikishwa kwenye majukwaa mbalimbali ya maamuzi kupitia mabaraza na vyama vya wazee.”amesema.
A nimeongeza kuwa, mambo mengi yameendelea kuwagusa wazee moja kwa moja ikiwemo huduma za matibabu bure kupitia vituo vya huduma na kambi za matibabu bure ambapo Arusha imekuwa mstari wa mbele wa msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid ambapo wazee walinufaika kwa kiwango kikubwa hususani waliokuwa wamedhulumiwa mali zao.
“Sisi wazee wa mkoa wa Arusha tunakushukuru Rais Samia kwa moyo wako mwema wa kuendelea kuhimiza mshikamano na amani katika mkoa wetu na umekuwa ukionyesha jambo hili kwa vitendo kwa kuyahusisha makundi mbalimbali .”amesema.
Ameongeza kuwa, katika kuendelea kusimamia maslahi ya wazee na Taifa kwa ujumla amesisitiza jamii kuendelea kuziishi na kuzitunza tunu za Taifa letu zilizoasisiswa na Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere.
Kisakeni amewaomba viongozi wa mila,dini,na jamii kuendelea kuhubiri amani,mshikamano na ustahilivu kabla , wakati na baada ya uchaguzi huku wakiitaka serikali kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani ya Taifa kwa sababu ya tofauti za kisiasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa wazee mkoa wa Arusha ,Emmanuel Munga amesema kuwa ,wana imani kubwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuwa masuala ya wazee ikiwemo pensheni kwa wote ,bima ya afya kwa wote, na ushirikishwaji katika nyanja zote vitaendelea kupewa kipaumbele.