Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU)Crisipin Chalamila wa tatu kushoto,akikabidhi mashine maalum kwa ajili ya wodi ya watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wanaozaliwa kabla ya wakati na ugonjwa wa manjano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma,kushoto kwake Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Majura Magafu,kulia Daktari wa kitengo cha watoto Dkt Regina Hyera na wa pili kulia Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Crispin Chalamila kushoto,akiagana na Mganga Mfawidhi wa Hospitaliya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma(Homso) Dkt Majura Magafu baada ya kukabidhi mshine maalum kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wenye changamoto mbalimbali,katikati Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Luis Chomboko.
……….
Na Mwandishi wetu Songea
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU),imetoa msaada wa mashine ya joto na mashine ya kutibu homa ya manjano kwa watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati(njiti)wale wenye homa ya manjano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma(Homso).
Akikabidhi mashine hiyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa Songea Dkt Majura Mgafu, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila alisema, mashine hizo zimenunuliwa na wafanyakazi wa Takukuru kupitia michango wanayotoa kila mwaka kama sehemu ya kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum kama vile huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema,vifaa hivyo ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha huduma za afya kwa Watanzania na kuwataka wafanyakazi wa Hospitali hiyo kutunza vifaa hivyo ili viweze kusaidia katika kutoa huduma bora kwa watoto wachanga.
“Serikali inaleta fedha,dawa na vifaa tiba hivyo ni wajibu wenu watumishi kuhakikisha mnatumia vifaa na fedha kama ilivyokusudiwa bila kudokoa,sisi tuna wajibu wa kufuatilia fedha ili kuona kama zinatumika kama inavyotakiwa”alisema Chalamila.
Chalamila alisema,Takukuru ni Taasisi yao hivyo wanapaswa kuitumia kikamilifu kwani watumishi wa afya wanafanya kazi ili kuhakikisha wanaimarisha na kuboresha afya za Watanzania na Takukuru ina kazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwemo miradi ya afya.
Alisema,Takukuru ipo tayari wakati wote kushirikiana na Hospitali ya Rufaa Songea ili kuona miradi inayotekelezwa katika Hospitali hiyo na nyingine hapa nchini inatekelezwa vizuri bila kuwepo vitendo vya ubadhilifu na udokozi ili ikamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma inayostahiki.
“Mganga Mkuu wa Mkoa,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa na watumishi wengine,sisi tuko tayari kuja ili kushirikiana na na nyinyi wakati wote,lakini hata msipotualika tutajialika wenyewe ili kuona mambo yanavyokwenda ili malengo mazuri ya Serikali yetu na Rais wetu katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania wote yaweze kufikiwa”alisema.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda alisema,vifaa hivyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Takukuru na Hospitali ya Rufaa ambapo wamekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa idara ya afya katika vituo vyote vya afya vilivyopo katika Mkoa huo.
Mwenda alitaja eneo linguine la ushirikiano kati ya Takukuru na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ni kwenye ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta ya afya na katika kaguzi zote zilizofanywa kwenye miradi Hospitali ya Rufaa hiyo inatoa ushirikiano mkubwa.
Alisema, hata mapendekezo yanayotolewa yanatekelezwa kwa ukamilifu na uadilifu mkubwa na ushirikiano kati ya Takukuru na Homs oni mkubwa na umekuwa ukiimarika na msaada wa vifaa vilivyotolewa na wafanyakazi wa Takukuru vitazidi kuimarisha uhusiano kati ya Taasisi hizo.
Awali Daktari Bingwa wa watoto wa Hospitali ya rufaa Songea Regina Hyera alisema,Hospitali ya rufaa Songea inatoa huduma kwa wagonjwa waliopewa rufaa kutoka Hospitali za Halmashaur zote nane za Mkoa wa Ruvuma na wale wa maeneo Jirani ambao hwajapata rufaa.
Hyera alisema,kitengo cha Watoto ina wodi mbili ambazo ni wodi ya Watoto wachanga ambayo inatoa huduma kwa mtoto tangu anapozaliwa hadi anapofikisha siku 28 na wodi ya Watoto wenye umri zaidi ya mwezi mmoja.
Alisema,wodi ya Watoto wachanga inatoa huduma za matibabu kwa Watoto wenye matatizo mbalimbali kama vile Watoto waliochelewa kulia wakati wa kuzaliwa,uti wa mgongo, kichomi, manjano,maambukizi ya bakteria kwenye mfumo wa hew ana wale wenye uzito mdogo(njiti),upungufu wad amu na ulemavu wa viungo.
Hyera alieleza kuwa, huduma nyingine zinazotolewa ni kutunza Watoto wachanga ambao hawana changamoto za kiafya, lakini wazazi wao na wale ambao wamepoteza wazazi wanapata huduma mbalimbali.
“Watoto hawa wanapata huduma kama vile dawa,usaidizi wa kupumua, kwa njia ya tiba hewa(Oxygen)kutibu manjano kwa mashine maalum,kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa,kulishwa,kutunza joto la mwili kwa mashine na usafi wa mwili”alisema.
Alisema,kwa wastani wodi hiyo inahudumia watoto 60 hadi 90 kwa mwezi,hivyo kwa mwaka mzima watoto wachanga takribani 800 hadi 1,000 na takwimu zinaonyesha mwaka 2023 hadi 2024 watoto wachanga 1,974 wenye changamoto mbalimbali walilazwa katika wodi hiyo.
Alisema,kati yao 434 sawa na asilimia 22 walikuwa wamezaliwa na uzito mdogo(njiti) na 73 sawa na asilimia 4 walikuwa na ugonjwa wa manjano na mwaka 2025 kuanzia Mwezi Januari hadi Septemba jumla ya Watoto wachanga 609 walilazwa.
Hyera alisema, Watoto 261 sawa na asilimia 43 walikuwa njiti na 62 sawa na asilimia 10 walikuwa na manjano hali inayoonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la Watoto njiti na wenye ugonjwa wa manjano.