NA JOHN BUKUKU-CHATO
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Eziekiel Wenje, amejiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo, huku akimshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumpokea na kumkaribisha.
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wananchi na wanachama wa CCM waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais huyo, Wenje alisema kwamba ndani ya miaka 15 aliyokuwa kwenye siasa, alikuwa “anacheza ligi daraja la kwanza”, lakini sasa “ameingia ligi kuu.”
Alisema anashukuru kwa kupokelewa na kuingia rasmi kwenye chama hicho kikubwa hapa nchini, jambo ambalo lilikuwa ndoto yake ya muda mrefu na sasa imetimia, huku akiahidi kutoa ushirikiano wa dhati.
Aidha, Wenje alisema kwamba umefika wakati wa kutambua kuwa nchi ni kubwa kuliko mtu mmoja, na kwamba ametambua kazi kubwa iliyofanywa na CCM tangu uhuru, hasa katika kudumisha amani na utulivu ambao umeendelea kuwa chachu ya maendeleo nchini.
“Mhe. amani, utulivu na maendeleo makubwa ni msingi wa nchi hii. Leo nchi ikiwa na shida hakuna pa kukimbilia barabarani, hakuna bodaboda barabarani, hakuna mama mbogamboga barabarani. Kama kuna mtu anabisha, aende Sudan au ajaribu Somalia, ndipo ataelewa. Ndiyo maana mimi moyoni mwangu naamini wakati umefika kuhamia CCM,” alisema.
“Niwakumbushe, mwaka 2000 kule Uganda kulikuwa na kiongozi mmoja wa dini aliyeambia waumini wake wauze kila kitu waende mbinguni. Sasa leo mtu anakuambia Oktoba 29 muandamane, lakini yeye, mke wake na watoto wake wako Ujerumani — kipo kitu cha kujifunza hapo,” aliongeza.
“Mhe. Mwenyekiti, tunatambua duniani kote hakuna nchi iliyopata maendeleo ghafla. Maendeleo ni mchakato. Leo nimetoka Mwanza, nimesoma Geita. Zamani ukisafiri kutoka Mwanza kwenda Geita ulitumia saa 10, lakini leo ni muda mfupi sana kufika — hayo ni maendeleo makubwa,” alisema.
Hata hivyo, Wenje alisisitiza kuwa hakuna nchi wala serikali yoyote duniani inayoweza kuotesha maendeleo kama uyoga ndani ya miaka mitano au kumi, kwani maendeleo ni hatua kwa hatua na kazi inafanyika.
Akizungumzia suala la CHADEMA kudai kuwa wamezuiwa kushiriki uchaguzi mkuu, Wenje alisema hoja hiyo si ya kweli kwa sababu yeye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu hadi alipojiuzulu leo.
Alifafanua kuwa Januari 20 mwaka huu, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana jijini Dar es Salaam, ikafanya Baraza Kuu la chama, na baadaye mkutano mkuu ambao uliamua rasmi kutoshiriki uchaguzi.
“Kwa hiyo, nani ametuzuia tusishiriki uchaguzi wakati tulikubaliana wenyewe? Tumeweka mpira kwapani, tumeogopa. Walishambuliwa mpaka na wazee wa maana duniani walikutana na Raila Odinga, wakawaambia hakuna chama chochote kilichowahi kususia uchaguzi,” alisema Wenje.