Tarehe 7.10.2025 Mwenge wa Uhuru uliingia katika Mkoa wa Mbeya ukitokea katika Mkoa wa Songwe ambapo mapokezi yalifanyika katika mazingira ya usalama wa hali ya juu kutokana na ushirikiano tulioupata kutoka kwa wananchi wa Jiji letu la Mbeya.
Hadi sasa Mwenge huo umeshakimbizwa katika Wilaya zote tano na halmashauri sab ana kote huko hali ya ulinzi na usalama iliimarishwa kwa ushirikiano wa wananchi, Jeshi la Polisi na vyombo vingine pamoja na wadau mbalimbali.
Kesho 14.10.2025 mbio za Mwenge huo wa Uhuru zitahitimishwa hapa Jijini Mbeya ambapo utazimwa rasmi ikiashiria pia Sikukuu ya kumbukizi ya Hayati Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa.
Jiji la Mbeya limeshapokea wageni wengi na tunatarajia Viongozi wa Kitaifa kuwasili kwa ajili ya kushiriki shughuli hiyo ya Kitaifa ya kuhitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi wa Jiji kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa Pamoja kuendelea kuimarisha utulivu na usalama ili sherehe hizo ziweze kufanyika na kumalizika kwa amani.
Aidha, kutokana na wageni mbalimbali ambao wameshawasili na wanaoendelea kuwasili tunatoa wito kwa watumiaji wote wa barabara wazingatie sheria Pamoja na maelekezo watakayopewa na Askari Polisi ili misafara iweze kupita Salaam.
Pia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lingependa kuwahakikishia wananchi kuwa limejipanga vizuri kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama unaendelea kuimarika wakati wote wa shughuli za kuzima Mwenge wa Uhuru na baada ya shughuli hiyo kumalizika. Aidha, halitasita kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi wale ambao kwa makusudi watashindwa kutii sheria.