Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akiangalia dawa anazotumia Abdouloihid Idarouse mkazi wa kisiwa cha Ngazidja ambaye alifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundo dogo wa kuzibua mshipa wa damu wa moyo uliokuwa umeziba katika taasisi hiyo. Idarouse alifika katika hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan ambako madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wakiwemo wa JKCI walikuwa wanatoa huduma za matibabu kwa wananchi.
Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Gerson Mpondo akimkabidhi mkazi wa kisiwa cha Anjouan Soufiane Mohamed majibu ya kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania iliyokuwa inafanyika katika hospitali ya Hombo.
Daktari bingwa wa masikio, pua na koo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Julius Kessy akipima usikivu wa sikio la mtoto aliyefika katika Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwa cha Anjouan kwaajili ya kupata huduma za matibabu wakati wa kambi ya matibabu ya magonjwa mbalimbali iliyokuwa inatolewa na madaktari bingwa kutoka Tanzania.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mtoto aliyefika katika Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwa cha Anjouan kwaajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa kambi ya matibabu ya magonjwa mbalimbali iliyokuwa inatolewa na madaktari bingwa kutoka Tanzania.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan Dkt. Ibrahim Salim Mari mara baada ya kumaliza kwa kambi ya matibabu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wakiwemo wa moyo iliyokuwa inatolewa kwa wananchi. Picha na JKCI
……..
Na Mwandishi Maalumu – Anjouan, Comoro
Wagonjwa 852 wenye matatizo mbalimbali ya moyo wametibiwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenye kambi ya madaktari bingwa kutoka Tanzania iliyomalizia hivi karibuni katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro.
Akizungumzia wagonjwa waliotibiwa na taasisi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema kati ya wagonjwa 852 waliowaona watu wazima walikuwa 623 na watoto 229.
Dkt. Salehe alisema katika kambi hiyo wameona wagonjwa wenye matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, moyo kutanuka, matatizo ya valvu, moyo kushindwa kufanya kazi, shambulio la moyo, umeme wa moyo na matundu ya moyo kwa watoto.
Alisema kuwa tatizo la shinikizo za juu la damu ni kubwa ukilinganisha na matatizo mengine na watu wengi waliowaona hawakuwa wanafahamu kuwa wanatatizo hilo.
“Kati ya wagonjwa 852 tulionaona wagonjwa 92 wanahitaji kufanyiwa upasuaji mdogo na mkubwa wa moyo na wengine wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yao, hawa wote tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu”.
“Kuna wagonjwa ambao wanatibiwa katika taasisi yetu baada ya kusikia tupo Anjouan walikuja kliniki hawa nao tumewaona, tumewafanyia vipimo vya moyo na kuona maendeleo yao na wengine tumewabadilishia dawa za kutumia”, alisema Dkt. Salehe.
Dkt. Salehe alisema kambi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani kuna wagonjwa wamekutwa na shida za moyo na hawana uwezo wa kwenda kutibiwa Tanzania, hao wote wametibiwa na kupewa dawa za kutumia ambazo zilikuwa zinatolewa bila malipo na wataalamu kutoka Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).
“Katika kambi hii pia tumewajengea uwezo wataalamu wenzetu wa Hospitali ya Hombo ili wafahamu namna ya kuwatibu wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo kama shambabulio la moyo na moyo kushindwa kufanya kazi, tumewaelekeza namna ya kuwatibu wagonjwa hao na dawa nzuri za kuwapa ambazo zitasaidia kuokoa maisha yao”, alisema Dkt. Salehe.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara alisema kati ya watoto 229 aliowaona 10 walikutwa na matatizo yanayohitaji kufanyiwa upasuaji na hivyo kuwapa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Dkt. Nuru alisema watoto aliowakuta na shida za moyo walikuwa na matatizo ya valvu na matundu kwenye moyo wanahitaji kufanyiwa upasuaji ili wapone amewapa dawa wakati wazazi wao wanajipanga vizuri kifedha kwaajili ya kwenda kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Kambi hizi zina manufaa makubwa nimeona watoto waliokuwa na uhitaji wa kupata huduma za matibabu. Hospitali ya Pomoni ambayo nilikwenda pia kutoa huduma haikuwa na daktari wa watoto. Kuna watoto nimewaona hawana shida za moyo nimewakuta na matatizo mengine kama henia, nimewatibu na kuwapa dawa za kutumia”, alisema Dkt. Nuru.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Hombo Daniel Oiridi alisema uwepo wa kambi hiyo ya matibabu umekuwa na manufaa makubwa kwake pamoja na madaktari wengine wa hospitali hiyo kwani imewajengea uwezo zaidi katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.
“Kupitia kambi hii nimejifunza mbinu mbalimbali za kufanya vipimo bora vya moyo hususan kwa watu wazima, pamoja na namna ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo. Ushirikiano huu na wataalamu wa JKCI umetupanua uelewa na kuboresha huduma tunazotoa hapa Hombo” alisema Dkt. Oiridi.
Kwa upande wa wagonjwa waliotibiwa katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua afya zao na kuwapunguzuia gharama ambazo wangezipata kama wangeyafuata matibabu hayo Dar es Salaam.
“Mwaka jana katika kambi kama hii iliyofanyika kisiwani Ngazidja nilikutwa na tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI, nilikwenda Tanzania mwezi wa kwanza mwaka huu nikatibiwa na huduma niliyoipata ni nzuri ninashukuru”.
“Baada ya kusikia madaktari wa JKCI wako hapa nimekuja kuwaona ili nijue maendeleo ya afya yangu wamenifanyia vipimo vya moyo, ninamshukuru Mungu ninaendelea vizuri. Ninashukuru sana kambi hii ya matibabu ya madaktari bingwa kutoka Tanzania imenipunguzia safari ya kwenda Dar es Salaam”, alishukuru Abdouloihid Idarouse mkazi wa Ngazidja.
“Nilikuwa nikipata maumivu makali ya kifua kwa muda mrefu lakini sikuweza kwenda Tanzania kwa matibabu. Madaktari hawa waliponipima wamegundua nina tatizo la moyo na kunipatia dawa. Nashukuru sana kwa huduma hii ya huruma na upendo”, alisema Amina Abdallah mkazi wa Mutsamudu.
Wataalamu walioshiriki katika kambi hiyo ni kutoka katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Taasisi ya Saratani Ocean Road na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).