NA JOHN BUKUKU- CHATO
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mkoa wa Geita umeonyesha kasi kubwa ya maendeleo licha ya kuwa ni mkoa mchanga.
Akizungumza Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa EPZA Bombambili, mjini Geita, Dkt. Samia alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, serikali imewekeza nguvu kubwa katika huduma za kijamii, ujenzi wa miundombinu na mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi — hatua ambayo imeongeza ustawi wa wananchi na kuinua kipato chao.
Dkt. Samia alisema kuwa endapo ataendelea kupewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo, serikali itaendelea kuimarisha sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ambapo lengo ni kuona sekta hiyo inakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Alibainisha kuwa serikali inalenga kumuinua mkulima mmoja mmoja na kupitia ushirika, ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia vyema kwenye pato la taifa.
Amebainisha kuwa serikali itaendelea kuchanja mifugo, kujenga mabwawa, majosho na machinjio ndani ya mkoa huo ili kukuza sekta ya mifugo.
Katika kukuza ajira na uchumi wa viwanda, Dkt. Samia alisema serikali ya CCM itajenga viwanda vitakavyosindika mbegu za alizeti katika maeneo ya Bukoli na Busanda, huku kijiji cha Igate–Sungusira kikitarajiwa kupata kiwanda cha kusindika matunda. Amesema serikali inalenga kukuza sekta ya viwanda kitaifa kutoka asilimia 4.8 hadi 9.5 ifikapo mwaka 2030.
Kuhusu sekta ya madini, Dkt. Samia alisema kuwa Geita itajengewa maabara ya kisasa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ili shughuli zao zote zifanyike ndani ya mkoa huo bila kulazimika kusafiri nje. Aliongeza kuwa serikali inajiandaa kutoa mitaji kwa wachimbaji wadogo ili waweze kukua na kuwa wachimbaji wakubwa.
Pia, amebainisha kuwa serikali itajenga uwanja mkubwa wa kimataifa kwa ajili ya maonesho ya madini pamoja na uwanja wa mikutano ya sekta hiyo.
Katika sekta ya usafirishaji, Dkt. Samia alisema serikali itaendelea kuboresha barabara, kujenga vivuko vya kisasa na viwanja viwili vya ndege — kimoja mjini Geita na kingine wilayani Chato — ili kurahisisha usafiri na kuinua shughuli za kiuchumi.
Amebainisha kuwa serikali itaendeleza hifadhi za Bugiri na Rubondo kwa lengo la kukuza utalii, sambamba na kudhibiti wanyamapori waharibifu wanaoathiri mashamba na usalama wa wananchi.
Dkt. Samia alisema serikali itapima na kuwamilikisha wananchi ardhi katika maeneo ya wafugaji, miji na uwekezaji, ili kumaliza migogoro baina ya wananchi na serikali.
Akizungumzia sekta ya afya, alisema serikali imeendelea kuboresha huduma kwa kujenga hospitali za kibingwa na rufaa ndani ya mkoa wa Geita. Pia alitaja ujenzi wa tawi la Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) mkoani humo, litakalowawezesha wagonjwa wa moyo kupata matibabu bila kusafiri mbali.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali katika maeneo ambayo bado hayana huduma hizo, huku hospitali za wilaya zikiboreshwa kwa kujengewa majengo ya upasuaji na kuhifadhia maiti.