NA JOHN BUKUKU-CHATO
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuwa mlezi na mwalimu mzuri, kwani kazi zilizoanzishwa katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wake amezienzi na kuzifanikisha ipasavyo.
Dkt. Samia amesema, “Kazi tuliyoianza katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli nimeweza kuendelea nayo vizuri, kwa sababu alinielekeza vizuri na amenilea vyema, ndiyo maana nimeweza.”
Ameyasema hayo Oktoba 13, 2025, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Aidha, amebainisha kuwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alimuachia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ukiwa asilimia 37, na kwamba ameweza kulikamilisha, na hivi sasa taifa linavuna umeme kutoka bwawa hilo.
Amesema kuwa Reli ya Kisasa ya SGR iliachwa ikiwa zaidi ya asilimia 30 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, na sasa imekamilika huku wananchi wakisafiri kwa kutumia SGR, sambamba na kuendelea kujengwa kwa vipande vingine vya reli.
Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa mtangulizi wake aliacha ujenzi wa daraja la Kigongo–Busisi ukiwa asilimia 21, ambalo kwa sasa limekamilika na limefungua kanda hiyo kibiashara pamoja na nchi jirani.
Amebainisha kuwa Hayati Dkt. Magufuli aliacha mpango wa serikali kuhamia Dodoma, ambapo bunge na serikali vilitangulia kuhamia, na kwa sasa mhimili wa mahakama nao umeshahamia Dodoma.
Aidha, amesema kuwa Mji wa Kisasa wa Serikali ujulikanao kama “Magufuli City” upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Akizungumzia Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda, Dkt. Samia amesema kuwa mtangulizi wake aliliacha likiwa katika hatua za awali, na sasa liko karibu kukamilika, akisisitiza kuwa miradi mingi ya kitaifa iliyoanzishwa katika awamu ya tano imekamilika.
Aidha, amesema kuwa viongozi wengi waliopita wametekeleza maono na mawazo ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na serikali yake inaendelea kufanya hivyo ili kumuenzi.
Amesema kuwa ameanzisha miradi mipya na kuendelea kukamilisha miradi iliyokuwa imeanzishwa na Hayati Dkt. Magufuli, ili kumuenzi na kuendeleza jitihada zake za maendeleo.
Aidha, amesema kuwa Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Chato, ambayo ilianzishwa na Hayati Dkt. Magufuli, iliachwa ikiwa imeanza kujengwa, na chini ya uongozi wake amepeleka shilingi bilioni 48.4 ambazo zimesaidia kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Amesema kuwa mpango wa serikali ni kuifanya hospitali hiyo kuwa kituo cha umahiri wa tiba za kibingwa na kibobezi kwa magonjwa ya moyo kwa Kanda ya Kaskazini, ambapo wagonjwa wenye matatizo ya moyo watakuwa wanapatiwa matibabu hapo.
Katika sekta ya elimu, amesema kuwa Chuo cha Mafunzo na Usimamizi wa Fedha pamoja na Chuo cha Ufundi VETA vilivyoanzishwa na Hayati Dkt. Magufuli vimekamilika na vinaendelea kutoa mafunzo.
Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa serikali imekamilisha ujenzi wa stendi za mabasi za Chato na Kahumo ili kukuza biashara ya usafirishaji, na sasa zaidi ya mabasi 100 yanatoa huduma katika vituo hivyo.
Pia, amesema kuwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, zaidi ya shilingi bilioni moja imetolewa kwa vikundi 100 kupitia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, amesema kuwa katika miaka mitano ijayo serikali itatenga maeneo maalumu kwa wachimbaji wadogo wa madini ili wapate fursa zaidi za kujiendeleza kiuchumi.