JOHN BUKUKU-GEITA
Waziri wa Maji na Mgombea Ubunge wa Pangani, Jumaa Aweso, amesema kuwa katika vijiji 489 vya Mkoa wa Geita, upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 75. Amesema kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, upatikanaji wa maji uwe asilimia 100. Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 124 zimetolewa ili kufanikisha mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi kufika katika Mkoa wa Geita.
Amesema hayo Oktoba 13, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizofanyika mkoani Geita.
Aweso amebainisha kuwa mkandarasi yupo kazini kuhakikisha majimbo yote ya Geita yanapata maji kama ilivyoelekezwa na serikali. Amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi anayeishi kwa vitendo na kutimiza ahadi zake, akisema:
“Ndugu zangu wa Geita, najua mnahuzunika mmeondokewa na kaka yangu, lakini dada yenu nipo, sitawaacha Geita,” amesema Waziri Aweso.
Aidha, Aweso amenukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusema kuwa:
“Kiongozi hakumbukwi kwa cheo, bali anakumbukwa kwa namba ambazo ameziacha kwa maendeleo ya wananchi wake.”
Ameongeza kuwa taifa litamkumbuka Dkt. Samia kwa alama za maendeleo anazoendelea kuziacha nchini kupitia miradi mikubwa ya maji, barabara, elimu na afya.
Pia amewataka wananchi wa Geita na wanachama wote wa CCM kushikilia na kulinda mafanikio yaliyopatikana, akisema:
“Kiongozi aina ya Dkt. Samia hawapatikani kila wakati. Tumempata, lazima tumtumie kwa maslahi ya Watanzania,” amesema Aweso.
Aidha, amesisitiza kuwa:”Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mama mahiri na shupavu ambaye ameweza kulivusha taifa hili; tumpe heshima yake,” amesema Waziri Aweso.
Mwisho, Aweso amewataka wananchi wa Geita ifikapo Oktoba 29, 2025, kumpigia kura nyingi Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wote wa CCM ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.