Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Kwa lengo la kuielimisha jamii juu ya tahadhari dhidi ya majanga na namna ya kuyapunguza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani limeungana na Shirika la Msalaba Mwekundu kuadhimisha Siku ya Kupunguza Majanga Duniani, 13 Oktoba 2025.
Maadhimisho hayo yamehusisha utoaji wa elimu kwa wananchi na shughuli za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira, uchangiaji damu, na ugawaji wa misaada ya bidhaa muhimu kwa wahitaji.
Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika katika Manispaa ya Kibaha, Kamanda wa Zimamoto mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Jenifa Shirima alisema ,maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kuikumbusha jamii umuhimu wa maandalizi dhidi ya majanga kama moto, mafuriko, na majanga ya kiafya.
Shirima alitoa rai kwa jamii, kutumia vifaa vya umeme kwa usahihi, kuepuka kuwasha moto karibu na vitu vinavyowaka haraka, na kuwa na vifaa vya kuzimia moto majumbani.
“Kupitia siku hii, tunatoa ujumbe muhimu kwa jamii juu ya kujiandaa, kuchukua tahadhari na kuchukua hatua mapema ili kupunguza madhara ya majanga” alieleza Shirima.
Aidha walishiriki kwenye usafi wa maeneo ya umma, na kutoa vifaa vya usafi kama sabuni, taulo za watoto na vifaa vya kujikinga na magonjwa kwa wenye uhitaji.
Amor Mohamed aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha, alilipongeza Jeshi la Zimamoto na wadau wake kwa juhudi hizo, akisema kuwa zinasaidia kuijenga jamii yenye uelewa na uwezo wa kukabiliana na majanga kwa ufanisi.
“Hatua hii inaonyesha moyo wa huruma na uzalendo, elimu na huduma zinazotolewa si za muda mfupi bali zina mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii yetu,” alisema.
Siku ya Kupunguza Majanga Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhimiza mataifa na jamii kuchukua hatua madhubuti za kupunguza madhara ya majanga na yale yanayosababishwa na shughuli zabinadamu.