NA JOHN BUKUKU
Mratibu wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera, Agrey Mwanri, amesema kuwa wananchi wa mikoa hiyo wamejipanga kuhakikisha Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Amesema kuwa timu yao inaongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na kwamba kutokana na majukumu mengine ya kitaifa, Waziri Mkuu amewaomba wamwakilishe katika majukumu ya kampeni za chama hicho.
Aidha, Mwanri amebainisha kuwa mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera imekuwa na mshikamano mkubwa na imani thabiti kwa Dkt. Samia kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema kuwa viongozi wa CCM katika kanda hiyo wamezunguka katika mikoa yote mitatu na kujionea mafanikio ya Serikali, ikiwemo ujenzi wa shule, madawati kwa wanafunzi, pamoja na miradi ya kimkakati kama bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.
Mwanri amesema kuwa wananchi katika maeneo hayo wameahidi kumpigia kura Dkt. Samia kwa wingi, akisisitiza kuwa “wakati wa kupiga kura mbili mbili hautoshi, bali kura zote lazima ziwe za kishindo.”
Amebainisha kuwa wananchi wana imani kubwa na uongozi wa Dkt. Samia kutokana na kazi kubwa ya kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya Watanzania, huku akiwataka wana CCM kuendelea kudumisha umoja na mshikamano hadi siku ya uchaguzi.
Pia, Mwanri amewataka wananchi wa mikoa hiyo kuendelea kumuombea Dkt. Samia, ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa manufaa ya Taifa zima.